Suala la mabadiliko ya tabia nchi lapewa kipaumbele Davos

Viongozi wanaokutana katika Kongamano la Kimataifa la Kiuchumi mjini Davos, Uswisi, wamelipa kipau mbele suala la kushinikiza kuimarishwa uchumi wa ulimwengu na kupunguza kiwango cha joto duniani kwa kuzingatia vyanzo safi vya nishati. 
Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, Christiana Figueres, amesema uchumi wa ulimwengu uko hatarini, kama hapatakuwepo na muafaka mjini Paris mnamo mwaka wa 2015 wa kupunguza kiwango cha gesi ya sumu kutoka kwenye makaa ya mawe na mafuta.
Mkutano huo ambao umeng'oa nanga hii leo, unahudhuriwa na zaidi ya viongozi 40 wa nchi na serikali pamoja na mawaziri wengi wa mambo ya kigeni kutoka kote ulimwenguni. 
Kwa mara ya kwanza katika mwongo mmoja, Rais wa Iran, Hassan Rouhani, atapewa fursa ya kulihutubia kongamano hilo hapo kesho. 
Rouhani anatarajiwa kuzungumza kuhusu mpango wa nchi yake wa nyuklia pamoja na nafasi za uwekezaji kwa makampuni ya kigeni.