AU yaisifia IGAD inavyoshughulikia mgogoro wa Sudan Kusini


Wajumbe kutoka upande wa waasi wakiwa Ethiopia kwenye mazungumzo ya kutafuta amani Sudan Kusini
Wajumbe kutoka upande wa waasi wakiwa Ethiopia kwenye mazungumzo ya kutafuta amani Sudan Kusini
Naibu mwenyekiti wa Umoja wa Afrika-AU anasema taasisi yake  inafanya kazi na washirika  wa kimataifa kuweka shinikizo kwa pande  hasimu za Sudan Kusini kubuni eneo la kibinadamu ambalo litaruhusu mashirika ya misaada kugawa  misaada zaidi inayohitajika kwa waathirika wa mgogoro.

Sikiliza sauti ya ripoti hii

Erastus Mwencha aliiambia Sauti ya Amerika-VOA kuwa AU pia inahamasishwa na juhudi za IGAD kwenye mazungumzo ya amani yanayoendelea nchini Ethiopia ya kusaidia kurejesha hali ya usalama huko Sudan Kusini. Mazungumzo yamekwama juu ya kuendelea kushikiliwa kwa wanasiana 11 walioshutumiwa na Rais Salva Kiir kwa kupanga kuiangusha serikali mjini Juba.

Makamu Rais wa zamani Riek Machar  hadi sasa anakataa kutia saini mkataba wa kusitisha mapigano akisisitiza kwamba maafisa waliokamatwa wanatakiwa kuachiwa kabla ya mkataba kutiwa saini. Mwencha anasema AU inaunga mkono juhudi za IGAD kusaidia kutatua masuala yanayodumaza mashauriano ya amani katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa.

Mamia ya wa-Sudan Kusini wamekoseshwa makazi kutokana na ghasia. Mwencha anasema kuna haja kwa pande zinazopambana kutoa fursa kwa makundi ya misaada ambayo yanaweza kutoa msaada kwa waathirika wa mgogoro.
                                                                                                    
                                                                                                      
Rais wa Uganda Yoweri MuseveniRais wa Uganda Yoweri Museveni
Wakati huo huo Uganda inakiri kuwa majeshi yake yanalisaidia jeshi la Sudan Kusini kupambana na waasi ikibadilisha ukanushaji wa awali. Msemaji wa jeshi la Uganda  alisema Alhamis  kuwa majeshi ya nchi yake yanasaidia kuwafurusha waasi kutoka Bor, mji mkuu wa jimbo la Jonglei, Sudan Kusini.

Awali Rais Yoweri Museveni alisema majeshi ya Uganda yalishiriki kwenye mapigano  makubwa na waasi siku ya Jumatatu kiasi cha kilomita 90 kutoka mji mkuu, Juba.  Uganda awali ilisema majeshi yake yalikuwepo huko Sudan Kusini kuwalinda na kuwaondoa raia wa Uganda. 
Na VioaSwahili