Serikali ya Ukraine yautetea muafaka wake na Urusi

Waziri Mkuu wa Ukraine Mykola Azarov ameutetea mkataba ambao nchi hiyo ilisaini na Urusi akisema umeiwezesha serikali kuepuka kufilisika pamoja na kusambaratika huduma za jamii.
 Azarov amesema muafaka huo uliotiwa saini na Rais wa Ukraine Viktor Yanukovych na mwenzake wa Urusi Vladmir Putin ulikuwa njia pekee ya kuuokoa uchumi wao uliokuwa umedorora kwa muda. Mapema leo, upinzani nchini Ukraine ulimkosoa rais Yanukovych ukisema anauza masilahi ya Ukraine kwa Urusi na kuinyima nchi hiyo nafasi ya kujiunga na Umoja wa Ulaya.
 Upinzani unahofia kuna mambo ya siri ambayo yalifungamanishwa na makubaliano hayo ya mkopo wa dola bilioni 15 pamoja na kuiuzia gesi Ukraine kwa bei ya chini. Kiongozi wa upinzani Vitali Klitschko ameahidi kuendelea kumshinikiza rais Yanukovych aitishe uchaguzi wa mapema.