DK GURNAH: ZANZIBAR ISIITUPE HISTORIA

 


MAALIM  wa skuli wa Zanzibar wa zamani,  Dk Ahmed Gurnah amesema ipo siku itafika Wazanzibari watasherehekea matukio makubwa ya Historia ya nchi yao, kwa ridhaa ya serikali kwa sababu Wazanzibari wamegawanyika makundi mawili kutokana na matukio hayo.
Pia, amesema kupinga na kuchukia ‘Uhuru wa Zanzibar’, uliyotolewa na Muingereza ni kujidanganya huku, tukio hilo linajuilikana duniani kote: “Mapinduzi yalifanywa baada ya Uhuru wa Desemba 10, 1963 na hilo si jambo la kukizana au kuchukiana,”.
Dk Gurnah alisema hayo mwishoni mwa wiki iliyopita mjini London, wakati akitoa ufafanuzi wa maswali mengi yalioulizwa juu ya ‘Uhuru wa Zanzibar na Mapinduzi ya mwaka 1964’.
Alisema katika matayarisho ya Uhuru wa Zanzibar, vyama vyote vikuu vya siasa ‘ZNP, ASP na ZPPP’ vilikutana ‘Lancaster House’ London, na mchakato mzima wa Uhuru ulikamilishwa na mkutano huo. ASP na ZNP ndiyo vyama vya siasa vikubwa Zanzibar, kwa wakati huo.
Dk Ahmed Gurnah, ambaye amewahi kusomesha ‘Oxford University’,  alialikwa na Jumuiya ya Wazanzibari wanaoishi nje (MUWAZA) katika Mdahalo wa kusherehekea ‘Uhuru wa Zanzibar’ katika hafla iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Durning, Forest Gate, East London, Jumamosi iliyopita.
Alisema katika uchaguzi mkuu wa mwaka 1961, Chama cha Afro Shirazi kilijenga matumaini makubwa ya kushinda uchaguzi kutokana na uwiano na nguvu iliyokuwa nayo ya kuungwa mkono na kila kabila iliyokuwapo Zanzibar:
“Linapokataliwa kukumbushwa tukio la Uhuru wa Desemba 10, 1963 ni sawa na kusema ‘Afro Shirazi Party’ haikushiriki katika mchakato wa kudai Uhuru wa Zanzibar kutoka kwa Muingereza…na huko ni kuidhalilisha Afro Shirazi,” alisema na kuongeza:
“Bila kuukumbusha Uhuru na kuwasomesha vijana wa sasa matukio hayo, Historia itakuwa imepotoshwa na kuonekana kana kwamba Afro Shirazi kilikuwa kikundi cha wahuni kilichokuwa kikifanya shughuli zake msituni na kuibuka kwa kufanya Mapinduzi jambo ambalo si sahihi,” alisema Dk Gurnah.
Hata hivyo, alisema anaamini kwamba siku za mbele serikali itaridhia kufanyika kumbukumbu za Uhuru huo kwa sababu wapo watu wanaopenda kushrehekea na wapo wanaopenda kusherehekea Mapinduzi:
“Ni busara matukio yote mawili yakaadhimishwa madam watu wanapenda wala hakuna ubaya…Ghana na Nigeria  wamepinduana sana na mataifa mengine ya Afrika lakini wanasherehekea Uhuru…Mapinduzi ni tukio la mpito,” alisema Dk Gurnah.
Alisema Afro Shairazi ni miongoni mwa vyama vilivyodai Uhuru wa Zanzibar, na kilipaswa kuikumbuka siku ya Uhuru sambamba na Mapinduzi, hata kama hakikuweza kuunda serikali lakini, kinahusika na tukioa hilo.
Katika hatua nyingine, Jumuiya ya Wazanzibari Wanaoishi Nje (MUWAZA) kufuatia mdahalo huo, walipitisha azimio la kuendeleza kusherehe Uhuru wa Zanzibar, kila mwaka.
Aidha, walitaka kuendelezwa kwa Umoja na mshikamano wa Wazanzibari, ili kuweza kuviletea maendeleo visiwa vya Unguja na Pemba, kwa kuondoa tofauti zilizopo sasa, hasa za kisiasa na ukabila:
Azimio la MUWAZA, pia lilisema:  “Miaka 50 inatosha kutufundisha ‘mazuri na mabaya’ yaliyotendeka kuanzia mwaka 1964, na sasa Wazanzibari wote tunapaswa kusahau tofauti zetu na kusameheana kwa yaliyopita,” .
Mdahalo wa MUWAZA, ambao ulifanyika kwa lengo la kuadhimisha miaka 50 ya uhuru wa Zanzibar, ni wa kwanza kuhudhuriwa na watu wengi, pamoja na wageni pia, ulishirikisha Wazanzibari wanaoishi Germany, France na Denmark..
Na mzarendo.net