Showing posts with label 2017 at 02:33PM. Show all posts
Showing posts with label 2017 at 02:33PM. Show all posts
UAMUZI WA KIKAO CHA KAMATI YA UTENDAJI KUHUSU UCHAGUZI MKUU WA TFF

UAMUZI WA KIKAO CHA KAMATI YA UTENDAJI KUHUSU UCHAGUZI MKUU WA TFF

Kamati ya Utendaji (EXCOMM) ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania, ilikutana tena Jumanne Julai 4, 2017 katika kikao cha dharura ambako ilijadili mgawanyiko katika Kamati ya Uchaguzi ya TFF.
Kamati hiyo ya utendaji inakutana kwa dharura kwa mujibu wa Ibara ya 35 (1) ya Katiba ya TFF inayosomwa pamoja na Ibara ya 35 (6). Kikao cha Kamati hiyo kilianza saa 8.58 alasiri hadi saa 10.51 jioni.
Katika kikao chake kilichofanyika katika Ukumbi wa Ofisi za shirikisho, Karume jijini Dar es Salaam Kamati iliamua kufanya mabadiliko madogo katika Kamati zake za Kisheria na Kamati za uchaguzi kwa mujibu wa Katiba Ibara ya 44 (7) na Ibara ya 52 inayotoa mamlaka ya kufanya mabaduiliko hayo.
Katika Kamati ya Uchaguzi, EXCOMM imeteua Mawakili kuongoza kamati hiyo wakiongozwa na Msomi Wakili Revocatus Kuuli; Mheshimiwa Wakili Mohammed Mchengelwa; Msomi Wakili Malangwe Mchungahela; Msomi Wakili Kiomoni Kibamba na Msomi Wakili Thadeus Karua.
Katika Kamati ya Rufaa Uchaguzi, EXCOMM imeteua Msomi Wakili, Abdi Kagomba kuwa Mwenyekiti wakati Makamu Mwenyekiti ni Msomi Wakili Kenneth Mwenda na wajumbe ni Msomi Wakili Rashid Sadalla, Mhe. Jabir Shekimweri na Mohammed Gombati.
Kadhalika katika kamati za kisheria za TFF, ikianzia Kamati ya Maadili, EXCOMM imeteua Msomi Wakili Hamidu Mbwezeleni kuwa Mwenyekiti wakati Makamu Mwenyekiti ni Msomi Wakili Steven Zangira na wajumbe ni Mhe. Glorius Luoga, Walter Lungu na Amin Bakhressa.
Kamati ya Rufaa na Maadili, EXCOMM imeteua Msomi Wakili Ebenezer Mshana kuwa Mwenyekiti wakati Makamu Mwenyekiti ni Naibu Kamisha katika Jeshi la Polisi (DCP), Mohammed Mpinga na Wajumbe ni Msomi Wakili Benjamin Karume; Dk. Lisobine Kisongo na Mrakibu Msaidizi wa Polisi – ASP Benedict Nyagabona.
Kamati ya Nidhamu ya TFF, EXCOMM imeteua Tarimba Abbas kuwa Mwenyekiti wakati Makamu Mwenyekiti ni Peter Hella huku Wajumbe wakiwa ni Boniface Lyamwike, Dk. Billy Haonga na Kassim Dau.
Kamati ya Rufaa ya Nidhamu, EXCOMM imeteua Msomi Wakili Rahim Shaban kuwa Mwenyekiti wakati Makamu Mwenyekiti ni Siza Chenja huku Wajumbe wakiwa ni Abbas Mtemvu; Amani Mulika, Amin Bakhressa na Stella Mwakingwe.
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA
ASANTE KWA KUTEMBELEA MTANDAO WETU!!

from Blogger http://ift.tt/2sLx4y9
via IFTTT


BUNGE LIMEPITISHA MUSWADA WA SHERIA YA HUDUMA YA MSAADA WA KISHERIA

BUNGE LIMEPITISHA MUSWADA WA SHERIA YA HUDUMA YA MSAADA WA KISHERIA

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo, Mjini Dodoma limepisha Muswada wa Sheria ya Huduma ya Msaada wa Kisheria wa Mwaka 2016 (The Legal Aid Bill, 2016).
Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Harrison Mwakyembe alipokuwa akitoa taarifa wakati wa kuwasilisha muswada huo amesema kuwa muswada huo wa sheria umepitia hatua nyingi na umechukua muda mrefu hadi kufikia hatua ya kujadiliwa na Bunge tukufu.
Aliendelea kwa kusema kuwa muswada huo unapendekeza kutungwa kwa sheria ya msaada wa kisheria kwa lengo la kuanzisha (kwa mara ya kwanza katika histori ya nchi) mfumo wa kisheria wa kusimamia, kuratibu, kurasimisha na kutambua utoaji wa huduma ya msaada wa kisheria katika mashauri yote ya Jinai na Madai kwa mahitaji.
Aidha utaratibu uliokuwepo kwa miaka mingi kwa upande wa Serikali unahusu baadhi tu ya makosa ya Jina, makosa yenye adhabu kubwa kama vile ya kunyongwa hadi kufa na vifungo virefu. Ambapo huduma hiyo imekuwa ikitolewa katika ngazi ya Mahakama Kuu pekee na kwa wigo mdogo tu pale inapohitajika kwa maslahi ya haki na kwa maelekezo ya Jaji Mkuu au yeyote aliyekasimiwa mamlaka ya kutoa maelekezo hayo.
“Kumekuwepo na ongezeko kubwa la mahitaji ya huduma ya msaada wa kisheria na wasaidizi wa kisheria. Kutokana na hali hiyo, Serikali imeona ulazima wa kuanzisha mfumo wa kusimamia na kuratibu utoaji wa huduma hiyo ili kuhakikisha inatolewa na watu wenye sifa, kwa wahitaji halisi na kwa taratibu zinazofahamika ili iendane na matakwa ya kikatiba,” alifafanua Dkt. Mwakyembe.
Vile vile ameeleza kuwa muswada huo unalenga kuwatambua wasaidizi wa kisheria, kufuta sheria ya msaada wa kisheria (katika mashauri ya Jinai).
Kwa upande wake Mbunge Selemani Zedi amesema kuwa, muswada huo utawasaidia wananchi ambao hawana uwezo wa kuwalipa Mawakili wanapohitaji msaada wa Kisheria.
Aidha, Naibu Spika Dkt. Tulia Ackson ameipongeza Serikali kwa muswada huo muhimu ambao Bunge umeipitisha unasuobiria kutiwa saini na Mhe. Rais ili kuwa Sheria.

from Blogger http://ift.tt/2pp4cKD
via IFTTT


UMOJA WA WANAWAKE (UWT) WAMSHUKIA MWENYEKITI CHADEMA, FREEMAN MBOWE

UMOJA WA WANAWAKE (UWT) WAMSHUKIA MWENYEKITI CHADEMA, FREEMAN MBOWE

Jumuiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) unatoa pongezi kwa Wabunge wa Bunge Tukufu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutumia haki yao ya kidemokrasia, kikatiba na kikanuni kufanikisha uchaguzi wa Wabunge wa Afrika Mashariki uliofanyika tarehe 4/4/2017 bungeni mjini Dodoma.
Pia unawapongeza Wabunge waliochaguliwa kuiwakilisha nchi yetu katika Bunge la Afrika Mashariki, tunawataka kuwa wazalendo, waadilifu, wachapakazi na wenye kutanguliza maslahi ya nchi yetu Tanzania kwanza.
Pia, UWT imeridhishwa na hatua za mchakato wa uchaguzi huo ndani ya Bunge na inapongeza demokrasia pana, komavu na shirikishi iliyooneshwa na wabunge kwa kupiga kura ya HAPANA kwa wagombea waliotokana na CHADEMA kwa sababu uteuzi wao haukuzingatia misingi ya demokrasia, uwakilishi wa Kitaifa wala jinsia.
Uteuzi uliofanywa na CHADEMA hata baada ya kushauriwa, unadhihirisha dharau kubwa na kutothamini mchango wa Wanawake wa Tanzania katika maendeleo ya nchi yetu.
Bunge na Wabunge lazima wawe mstari wa mbele katika juhudi za kuimarisha demokrasia yetu kama Taifa na ndani ya vyama vya siasa, kamwe Bunge lisiruhusu kutumika kama “rubber stamp” kama ambavyo CHADEMA walipanga kwa kuteua wagombea wawili pekee na kwa kufanya hivyo tayari waliamua nani awe mbunge na kulinyima Bunge fursa na uhuru wa kuchagua miongoni mwa wagombea.
Aidha, UWT imesikitishwa sana na kauli za MATUSI, DHARAU na KEJELI alizozitoa Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni na Mwenyekiti wa CHADEMA Mhe Freeman Mbowe dhidi ya Wabunge na Bunge Tukufu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kitendo cha Mhe. Mbowe kuwatukana Wabunge sio tu kinakiuka Kanuni za Maadili ya Viongozi lakini pia kinatweza UTU na HESHIMA ya wabunge na bunge mbele ya jamii.
UWT inaungana na Maamuzi ya Mhe. Spika ya Kuwaita watovu wa nidhamu kwenye Kamati ya Maadili.Hata hivyo tunamtaka Mhe. Freeman Mbowe kuomba radhi wabunge na Umma wa Tanzania kwa lugha isiyo na staha.
Pamoja na kuomba radhi, tunamtaka Mhe Mbowe afute kauli yake ya kuwahusisha na kuwatuhumu Viongozi wa Serikali (Rais na Waziri Mkuu) na Viongozi wa Chama Cha Mapinduzi kuwa wameingilia uchaguzi wa wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki ndani ya Bunge.
UWT inaendelea kuwahimiza Wabunge kujadili na kupitisha Bajeti kwa kuzingatia vipaumbele muhimu kwa Maendeleo ya Jamii na Ukuaji wa Uchumi ikiwemo Ujenzi wa Miundombinu ya Maji, Afya, Elimu, Umeme Vijijini, pamoja na kuimarisha njia za Uchukuzi na Mawasiliano k.v Barabara na Reli.
KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI.
AMINA MAKILAGI
KATIBU MKUU
UMOJA WA WANAWAKE TANZANIA {UWT}
05 April, 2017.

from Blogger http://ift.tt/2o51bjo
via IFTTT


Kategori

Kategori