Dodoma. Wabunge jana
waliumbuana kuhusu matumizi mabaya ya fedha za umma huku Kiongozi wa
Kambi ya Upinzani, Freeman Mbowe akituhumiwa kuagiza kubadilishwa kwa
tiketi ya ndege ya Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Joyce Mukya ili
afupishe ziara yake ya kikazi huko Marekani na kwenda Uarabuni kwa
shughuli binafsi.
Mbali ya Mbowe, Mbunge wa Mbozi Mashariki, Godfrey
Zambi (CCM) anadaiwa kuchukua posho ya Kamati ya Hesabu za Bunge (PAC),
kwa safari ya kwenda Dubai na wenzake lakini badala yake akaenda Mbeya
kwenye ziara za chama chake.
Malumbano hayo yaliibuka jana baada ya Mbunge wa
Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba (CCM), kuomba mwongozo wa Spika
akitaka kufahamu kauli ya ofisi yake kwa Mbowe kutumia nafasi yake
kumrudisha mbunge ambaye ameshatumia fedha za Serikali.
Alidai kwamba Mbowe aliagiza Mukya aanze safari
Desemba Mosi, mwaka huu kutoka New York, Marekani ili aende Dubai, Falme
za Kiarabu (UAE) kabla ya kwenda Dar es Salaam, Desemba 3, mwaka huu.
Alipoulizwa kuhusu tuhuma hizo jana, Mbowe alisema
hawezi kuzungumza chochote kwa kuwa hakuwapo bungeni akisema alikuwa
Dar es Salaam kwenye kikao.... “Siwezi kusema lolote mpaka nipate
hansard (kumbukumbu rasmi ya Bunge) na kutoka kwa wabunge wangu walioko
Dodoma kujua nini kimesemwa.”
Akiomba mwongozo Nchemba ambaye pia ni Naibu
Katibu Mkuu wa CCM alisema: “Jambo hili limechukua taswira kama ni Bunge
lote linafanya mambo haya na limevunja heshima ya Bunge. Jambo hili
linatuvunjia heshima hata watu ambao tuna maadili ya uongozi na
tunaliheshimu taifa letu...
“Pamoja na kuwa jambo hilo lilikuwa la binafsi,
lakini kuna ujumbe tumeupata kuwa Kiongozi wa Kambi ya Upinzani amemzuia
mbunge wake kusafiri na magazeti yakaandika kwamba wana mahusiano. Mimi
sipendi kwenda kwenye uhusiano, nataka kwenye taswira ya Bunge na
Taifa.”
Alisema Bunge linapopanga safari za wabunge linazingatia wa chama tawala na wapinzani ili kuweka uwakilishi.
Nchemba alisema Mbowe ambaye pia ni Mwenyekiti wa
Chadema, aliandika ujumbe mfupi wa simu kwa mtumishi mmoja wa Bunge
akitaka kubadilishwa kwa tiketi ya ndege ya mbunge.
Aliusoma ujumbe huo: “Rejea mazungumzo yetu bwana
Kabunju kuhusu mheshimiwa Joyce Mukya ambaye yupo safarini. Nitashukuru
kama utambadilishia booking (safari) yake ili aweze kurudi, aondoke New
York tarehe moja Desemba na kurejea Dubai baadaye ataunganisha kurejea
Dar es Salaam by Mbowe kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni nakala kwa
Joyce Mukya.” Kabunju S. Kabunju ni Ofisa wa Bunge anayeshughulikia
masuala ya usafiri.
Nchemba alisema: “Ameshakatiwa tiketi, ameziba
nafasi ya kwenda kuliwakilisha taifa kule, anamwita arudi Dubai na ni
mbunge viti maalumu. Je, hili lina taswira gani kwa taifa na kiti chako
kinatoa kauli gani kwa watu ambao wanakwenda kutumia fedha za Serikali
kwa mambo binafsi, Dubai?” alisema.
Pia alitaka kufahamu Bunge linachukua hatua gani
stahiki kwa mbunge anapoingilia kazi za kiti na pia watumishi
wanapoingiliwa na kubadilisha yale waliyotumwa kwa ajili ya Serikali.
Na Mwananchi.com
Na Mwananchi.com