Rais wa Halmashauri ya Ulaya Jose Manuel Barroso ametoa wito wa kusitishwa machafuko nchini Ukraine na akaionya serikali ya nchi hiyo kuwa Kamati Kuu ya Umoja wa Ulaya itatathmini "uwezekano wa kuchukuliwa hatua".
Barroso amesema wameshtushwa na habari za karibuni kutoka Ukraine ambako waandamanaji wawili wameuawa mapema leo wakati polisi walipoivamia kambi moja ya maandamano na kuanza kupambana na waandamanaji wanaoipinga serikali.
Rais Viktor Yanukovich leo anakutana na viongozi wakuu wa upinzani, ikiwa ni siku moja baada ya kufutilia mbali uwezekano wa kufanya mazungumzo ya aina hiyo.
Wakati huo huo Waziri Mkuu wa Ukraine Mykola Azarov amewashutumu waandamanaji wanaoipinga serikali akiwaita kuwa ni "magaidi".
Maelfu ya Waukraine wamefanya maandamano mjini Kiev tangu rais Yanukovich alipokataa kusaini mkataba wa ushirikiano wa kibiashara na Umoja wa Ulaya, na badala yake akaimarisha mahusiano na Urusi.