Mkutano wa kimataifa unaolenga kuiondoa Syria katika mgogoro wa kivita, umeanza kwa majibizano makali huku suala la mustakabali wa Rais Bashar al-Assad likitishia kuyasambaratisha mazungumzo hayo hata kabla ya kushika kasi.
Mvutano kuhusu Assad lilikuwa suala kuu katika mkutano huo wa kimataifa uliofunguliwa rasmi mjini Montreux, Uswisi, ambao unalenga kuweka mkakati wa kuundwa serikali ya mpito na kisha kufanyika uchaguzi wa kidemokrasia katika nchi hiyo ya Mashariki ya Kati iliyoharibiwa na vita.
Mjumbe wa Marekani katika mkutano huo John Kerry, alianzisha kikao kwa kusema rais Assad alipoteza uhalali wake mara tu alipotumia nguvu kupita kiasi kuwakandamiza waandamanaji.
Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Syria, Walid al-Moalem, alijibu kwa ukali akisema kuwa ugaidi na uingiliaji wa kigeni vimeiharibu kabisa nchi hiyo.
Na wakati wajumbe wakiendelea kukabiliana kwa maneno, ndani ya Syria kwenyewe majeshi ya serikali na wapiganaji wa upinzani wamepambana katika maeneo ya Aleppo, Idlib na Daraa ambako maandamano ya kumpinga rais Assad yalianziia miaka mitatu iliyopita.