Merkel asema EU inastahili kuirekebisha mikataba yake

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema leo kwamba wanachama wa Umoja wa Ulaya lazima wawe wepesi wa kuifanyia mabadiliko mikataba ili kuimarisha uongozi wa pamoja wa kiuchumi katika umoja huo wenye mataifa 28. 
Merkel aliyasema hayo siku moja baada ya kuanza muhula wake wa tatu kama kansela wa taifa kubwa kiuchumi barani Ulaya, kabla ya kuelekea Paris kwa mazungumzo na Rais Francois Hollande. Baadae atakwenda Brussels kuhudhuria mkutano wa kilele wa siku mbili wa Umoja wa Ulaya unaoanza kesho. 
Bibi Merkel ameliambia bunge la Ujerumani kuwa Umoja wa Ulaya unahitaji kufanya kazi kwa kuzingatia uongozi wa pamoja wa kifedha na kiuchumi, ambapo wanachama wanaweza kushurutishwa kutimiza malengo kadhaa ya bajeti, hata kama kutahitajika mabadiliko katika mikataba muhimu ya Umoja huo. 
Rais Hollande wa Ufaransa anapinga kufanyiwa mabadiliko mikataba ya Umoja wa Ulaya, na badala yake anashinikiza kuwepo sera za kuwezesha ukuaji zaidi wa uchumi na kupunguza kiwango cha kubana gharama za matumizi ndani ya mikataba iliyopo
Na DW.DE