Rais wa Ukraine, Viktor
Yanu-kovich, amekubali ombi la kujiuzulu kwa waziri mkuu wa taifa hilo,
Mykola Azrov, pamoja na baraza zima la mawaziri licha ya hatua muhimu
kupigwa mnamo Jumanne.
Hata hivyo mawaziri hao waliojiuzulu wanasalia kuwa wasimamizi wa wizara zao hadi pale serikali mpya itakapo buniwa.Awali bunge la Ukrain lilipiga kura ya kuifutilia mbali sheria kali dhidi ya maandamano ambayo ilizua ghasia tangu iidhinishwe mwezi uliopita.
Kura ya kuifutilia mbali sheria hio ilipigwa na asilimia kubwa ya wabunge wa taifa hilo. Sheria hio ilipiga marufuku waandamanaji kutumia majengo ya umma pamoja na kuvaa vinyago.
Mwandishi wa BBC nchini Ukraine, amesema kuwa upinzani utaiona hatua ya waziri mkuu kujiuzulu pamoja na kufutilia mbali sheria inayozuia maandamano kama ushindi kwao
Mgogoro wa kisiasa nchini Ukraine, ulianza kama maandamano ya amani mwezi Novemba wakati ambapo Rais Yanukovych alipokataa kutimiza ahadi yake ya kushirikiana na Muungano wa Ulaya.
Waandamanaji hata hivyo wameapa kuendelea kuandamana hadi Rais Yanukovych atakapojiuzulu.
Na BBCSwahili