Shirika la habari la Urusi, Interfax, limemnukuu msaidizi wa rais wa nchi hiyo, Andrei Belousov, akisema kuwa Urusi huenda ikaipatia Ukraine mkopo, ikiwa utawala mjini Kiev utauomba.
Belousov alinukuliwa akisema hali imefikia mahala ambapo bila mikopo kutoka upande mmoja au mwingine, Ukraine itashindwa kuendeleza utulivu wa kiuchumi.
Wakati huo huo, kiongozi wa upinzani Vitali Klitschko, anasema wataandamana hadi waiangushe serikali.
Ukraine inatafuta msaada ili iweze kujaza pengo na ufadhili wa nje unaofikia dola za Marekani bilioni 17 mwaka ujao.
Rais Viktor Yanukovych wa Ukraine, ambaye amekabiliwa na maandamano tangu serikali yake ilipoamua kutosaini makubalinao ya biashara uhuru na Umoja wa Ulaya, anaizuru Urusi kesho Jumanne, na Belousov alisema huenda akaomba mkopo wakati wa ziara hiyo.