Human Rights Watch imeuomba pia Umoja wa Mataifa kuzuwia mali na kuwawekea vikwazo wale wote wanaohusika na uhalifu huo.
Shirika la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch, limesema mauaji ya raia kwa misingi ya ukabila yanayofanywa na vikosi vya serikali na waasi yamesambaa nchini Sudan Kusini.
Ripoti iliyotolewa na shirika hilo jana Alhamisi, ilisema uhalifu wa kutisha umefanywa dhidi ya raia, na kwamba uhalifu huo unaweza kufikia kiwango cha uhalifu dhidi ya ubinaadamu.
Mgogoro wa Sudan Kusini ulianza mwezi uliopita, baada ya rais Salva Kiir kumtuhumu aliekuwa makamu wake, Riek Machar kwa kufanya jaribio la mapinduzi.
Watu wanaokadiriwa kufikia 1,000 wameuawa katika mapigano kati ya wanajeshi watiifu kwa rais Kiir, na waasi wanaomuunga mkono Machar.
Siku ya Jumatano, Uganda ilithibitisha kuwa iliwatuma wanajeshi wake kupigana kwa upande wa vikosi vya serikali ya Sudan Kusini.
Na DW.DESwahili