Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir amesema wanajeshi wake wameukomboa mji
wa Malakal kutoka mikononi mwa waasi jana.(21.01.2014) Waasi
wameikanusha taarifa hiyo.
Msemaji wa waasi wa Sudan kusini aliyeko mjini Addis Ababa, Ethiopia ambako mazungumzo yanayolenga kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano yamekuwa yakisuasua, ametupilia mbali kauli ya rais Kiir. "Ni kweli wamejaribu kuuteka mji wa Malakal mwendo wa saa saba mchana lakini wameshindwa. Tungali tunaudhibiti mji huo," amesema Lul Ruai Koang, wakati alipozungumza na shirika la habari la Reuters.
Azimio lataka mapigano yasitishwe
Wakati hayo yakiarifiwa wapatanishi katika mkutano wa Addis Ababa wanazihimiza pande zinazopigana Sudan kusini kusaini mkataba wa kusitisha mapigano ili kuumaliza mzozo huo na machafuko yaliyoliharibu taifa hilo changa la Afrika. Hayo ni kwa mujibu wa rasimu ya makubaliano yaliyofikiwa kwenye mkutano huo.
Rasimu hiyo iliyoonekana na shirika la habari la AFP na kuwasilishwa kwa wajumbe, linataja kiwango cha mateso yanayowakabili raia, vifo vingi vilivyotokea, uharibifu wa mali na idadi kubwa ya watu kulazimika kuyakimbia makazi yao tangu mapigano yalipozuka Desemba 15 mwaka jana. Rasimu hiyo inapendekeza harakati zote za kijeshi zikome, na kuzitaka pande zote ziache kuwashambulia raia, kuua watu kiholela, kuwatumia watoto kama wanajeshi, ubakaji, udhalilishaji wa ngono na mateso.
Rasimu nyingine ya mapatano inamhimiza rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir awasamehe wafungwa 11 wa kisiasa, mojawapo ya masuala tete yaliyoyakwamisha mazungumzo hayo yanayosimamiwa na shirika la maendeleo la IGAD. Wafungwa hao wanatakiwa waachiwe ili washiriki kwenye mchakato wa maridhiano ya kitaifa.
Bashir kwenda Juba
Wakati huo huo, rais wa Sudan, Omar Hassan al Bashir, atasafiri kwenda Sudan Kusini Alhamisi wiki hii kuzipa msukumo juhudi za kutafuta amani. Hayo ni kwa mujibu wa shirika rasmi la habari la serikali, SUNA. Mualiko huo umetoka kwa waziri mkuu wa Ethiopia, Hailermariam Desalegn, mwenyekiti wa shirika la maendeleo la IGAD, ambalo linasimamia mazungumzo ya kusuluhisha mzozo wa Susan kusini. Ziara hiyo ya Bashir itakuwa ya pili kwenda Juba tangu mapigano yalipozuka katikati ya mwezi Desemba mwaka uliopita.