Umoja wa Mataifa umeonya juu ya hatari ya kutokea mauaji ya halaiki katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Taifa hilo lilitumbukia katika vurugu za kidini baada ya waasi wa Seleka kuchukuwa madaraka mnamo mwezi wa Machi mwaka 2013.
Wimbi la mauaji na uporaji katika Jamhuri hiyo lilisababisha mapigano kati ya Waislamu na wanamgambo wa Kikristu.
Zaidi ya watu milioni moja wamegeuzwa wakimbizi na mapigano hayo, na imeripotiwa kuwa zaidi ya alfu moja waliuawa katika mji mkuu Bangui pekee yake mwezi uliopita.
Afisa mwandamizi anaeshughulikia masuala ya kiutu katika Umoja wa Mataifa, John Ging, ambaye amerejea hivi karibuni kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati, amesema, hali inayoendelea huko ina dalili zote za mauji ya halaiki, kama zilizoshuhudiwa nchini Rwanda na Bosnia.
Kumekuwepo taarifa za ukosefu wa usalama tangu rais Michel Djotodia alipojiuzulu wiki iliyopita.
Na Dw.DeSwahili