Rais wa mpito wa Jamuhuri ya
Afrika ya Kati, Michel Djotodia, amejiuzulu kufuatia shinikizo kali na
kukosolewa kwa mwendo wake wa kujikokota katika kusuluhisha mgogoro wa
kidini unaotokota nchini humo.
Hatma ya Djotodia ilikuwa swala kuu katika ajenda ya mkutano wa viongozi wa kikanda kuhusu mzozo unaoendelea nchini humo.Maelfu ya watu waliandamana leo katika barabara za mji mkuu Bangui kumtaka Rais Djotodia, ajiuzulu.
Rais Djotodia amekosolewa vikali kwa kukosa kumaliza mapigano ya kidini kati ya wakristo na waliokuwa waasi waisilamu ambao walimsaidia kuingia mamlakani kwa njia ya mapinduzi mwaka jana.
Baraza lote la mpito katika Jamuhuri ya Afrika ya kati limekwenda nchini Chad ambako viongozi wa Afrika wanakutana kujadili mzozo unaoendelea nchini humo.
Mkutano huo wa viongozi wa kikanda, uliahirishwa, mapema asubuhi Ijumaa.
Lakini wajumbe kwenye mkutano huo wanasema walitakiwa kuendelea na mkutano usiku kucha ili kubuni mkakati kuhusu mustakabali wa Djotodia.
Viongozi wa kikanda wanasema wajumbe mia moja na thelathini na watano waliitwa kwa mkutano huo kwa sababu ni raia wa nchi hiyo pekee wanaoweza kuamua hatma ya taifa lao.
Ghasia baina ya wanamgambo wa kiisilamu na kikristo zimesababisha maelfu ya watu kuyahama makazi yao.
Djotodia aliingia mamlakani baada ya mapinduzi ya kijeshi mwezi Machi mwaka jana hali iliyotumbukiza taifa hilo katika viya vya wenyewe kwa kwenyewe.