Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa yuko Jamhuri ya Afrika ya
Kati katika juhudi za kukomesha mkondo wa umwagaji damu ambapo mamia ya
watu wameuwawa na asilimia 10ya wananchi wamepotezewa makaazi yao.
Watu waliopotezewa makaazi Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Balozi huyo wa Marekani kwa Umoja wa Mataifa Samantha Powers amesema
wakati wa mkesha wa ziara yake hiyo kwamba yeye na Rais Barack Obama wa
Marekani wana wasi wasi mkubwa na mauaji yanayofanywa na makundi ya
wanamgambo yanayohasimiana tokea serikali ya nchi hiyo ilipopinduliwa
hapo mwezi wa Machi. Amewaambia waandishi wa habari kwamba ghasia hizo
zimekuwa za kikatili na kimsingi zimeelekezwa dhidi ya raia na kuzidi
kuwa za madhehebu ambapo kunahitajika hatua ya dharura kuokowa maisha.Akitahadharisha dhidi ya kulinganisha Jamhuri ya Afrika ya Kati na maafa mengine ya nchi za Kiafrika mfano Somalia na Rwanda amesema wananchi wa Afrika ya Kati wako hatarini.Katika ziara hiyo Powers atakutana na viongozi wa kidini na wa kijamii pamoja na Rais Michel Djotodia.
Mataifa ya Ulaya yametowa msaada kusaidia kukomesha umwagaji damu huo wakati juhudi za Ufaransa za kuwapokonya silaha wapiganaji zikionekana kuzaa matunda kufuatia umwagaji damu huo uliozuka mapema mwezi huu.
Mvutano umepunguwa
Generali Francisco Soriano ambaye anaongoza vikosi vya Ufaransa nchini humo amesema hali ya mvutano imepunguwa sana na kumekuwa na utulivu katika mji mkuu wa Bangui tokea Ijumaa isipokuwa hawezi kusema iwapo hali hiyo itaendelea kudumu au la.
Shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadamu la Amnesty International limesema leo hii katika repoti kwamba wapiganaji wa Kiislamu katika mji mkuu wa Bangui wamewauwa takriban watu 1,000 katika kipindi cha siku mbili kulipiza kisasi kwa mauaji yaliofanywa na makundi ya vijana wa kujitolea wa Kikristo kwa wanaume 60 wa Kiislamu hapo Disemba tano.
Mauaji ya kisasi
Wahanga wa mauaji hayo ya kulipiza kisasi yaliofanywa na waasi waliokuwa wakiunga mkono serikali wa Seleka wengi wao walikuwa ni wanaume lakini pia walikuwemo wanawake na watoto na kwamba pia wanamgambo hao walifanya uporaji kwenye nyumba za raia. Mtaalamu wa Shirika la Amnesty kwa Afrika ya Kati Christian Mukosa amesema uhalifu umefanyika ukiwemo kunyongwa kwa watu, kukata viungo vya watu vipande vipande,uharibifu wa makusudi wa majengo ya kidini kama vile misikiti na kulazimisha mamia ya watu kuhama makaazi yao.
Kwa mujibu wa Amnesty licha ya kuwepo kwa vikosi vya Ufaransa na vile vya Afrika raia wameendelea kuuwawa kila siku ambapo takriban watu 90 wameuwawa tokea Disemba 8.Nayo ripoti ya shirika la Human Rights Watch imeonya kwamba vikosi hivyo vya Ufaransa vinapaswa kuimarishwa na vikosi kutoka nchi nyengine.
Mzozo huo wa Afrika ya Kati unatarajiwa kuwa juu katika agenda ya Mkutano wa Kilele wa Umoja wa Ulaya unaofanyika mjini Brussels leo hii na hapo kesho.