Mapigano bado yanaendelea Sudani Kusini

Watu waliokoseshwa makazi kufuatia mapigano huko Sudani Kusini wakiwa kwenye kambi ya ofisi za Umoja wa Mataifa-UNMISS Juba Dec. 22, 2013.
Watu waliokoseshwa makazi kufuatia mapigano huko Sudani Kusini wakiwa kwenye kambi ya ofisi za Umoja wa Mataifa-UNMISS Juba Dec. 22, 2013.

Wanajeshi waasi na majeshi ya serikali huko Sudan Kusini wanapigania udhibiti  wa mji wa Malakal, mji mkuu wa jimbo la Upper Nile lenye utajiri wa mafuta.

Mapambano katika mji huo yalianza Jumanne na kuendelea tena Jumatano, huku maafisa wa serikali wakikiri kuwa jeshi halina udhibiti kamili kwenye mji huo. Jumanne jioni baraza la usalama la Umoja wa Mataifa lilipiga kura kwa ajili ya kupeleka walinda amani 5,500 wa ziada huko Sudan Kusini ambako ofisa mmoja wa Umoja wa Mataifa, Toby Lanzer alisema inaonekana kuwa maelfu ya watu wameuwawa katika mapigano ya siku 10 zilizopita.

Mashahidi wanasema watu wengi wanalengwa kwa kuwa wanatoka kabila la Dinka au Nuer. Katika ujumbe wa mkesha wa sikukuu ya Krismas, Rais Salva Kiir alitoa wito kwa wa-Sudan Kusini kusitisha ghasia zote za kikabila.

Wakati huo huo  ofisi ya Umoja wa Mataifa huko Sudan Kusini inakanusha ripoti kwamba kaburi moja lenye miili ya watu wengi liligundulika huko Bentiu  mji mkuu wa jimbo la Unity linaloshikiliwa na waasi. Ofisi ya haki za binadamu katika Umoja wa Mataifa ilisema Jumanne kwamba miili ya hadi wanajeshi 75 wa kabila la Dinka iligundulika huko. Lakini ofisi ya Umoja wa Mataifa inasema ripoti ilikuwa inatofautiana na uhalisia ambao ulielezea kuwepo vifo vya kiasi cha watu 15.


John KerryJohn Kerry
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry aliwataka wote Rais Kiir na mpinzani wake  Makamu Rais wa zamani Riek Machar hapo Jumanne akiwasihi kusitisha mapigano na kufanya mazungumzo ya kisiasa.

Viongozi wote wawili wanasema wapo tayari kwa mashauriano lakini serikali inakataa madai ya Machar kwamba kwanza viongozi wa upinzani waliokamatwa waachiwe. Bwana Kiir anayetoka kabila la Dinka anamshutumu Machar kutoka kabila la Nuer kwa kupanga jaribio la mapinduzi mjini Juba hapo Disemba 15. Machar hajadai kuhusika na mapinduzi lakini anasema jeshi linatakiwa kumuondoa bwana Kiir madarakani.

Marekani inasema marine 150 wamepelekwa Djibouti tayari kuingia Sudan Kusini kuwaondoa wa-Marekani na kulinda maslahi ya Marekani. 
Na VOASwahili