Zoezi la upigaji wa kura ya maoni kuidhinisha katiba ya Misri limeendelea bila matukio yoyote mabaya leo baada ya mapambano ya jana na kusababisha watu 9 kuuwawa, ambapo watu waliojitokeza kupiga kura wanaonekana kuwa muhimu katika juhudi za mkuu wa jeshi kugombea kiti cha urais.
Waungaji mkono kadha wa rais aliyeondolewa madarakani Mohammed Mursi wamezuwia kituo cha treni ya mjini katika kitongoji kimoja cha mjini Cairo, wamesema maafisa wa usalama, lakini hakuna ripoti za kuvuruga upigaji kura.
Jana kumekuwa na mapambano ya hapa na pale katika sehemu kadha za nchi hiyo kati ya waungaji mkono wa Mursi na wapinzani wake pamoja na polisi na kusababisha watu tisa kuuwawa, na kuchafua zoezi hilo ambalo limekuwa kwa kiasi kikubwa likifanyika kwa amani.
Mursi rais wa kwanza wa Misri aliyechaguliwa kwa njia ya kidemokrasia na rais ambaye ni raia, aliondolewa madarakani na mkuu wa jeshi la Misri jenerali Abdel Fattah al-Sisi Julai mwaka jana kufuatia maandamano ya umma dhidi ya utawala wake uliodumu mwaka mmoja.
Na DW.DW