Rais wa Uganda, Yoweri Museveni,
amesema kuwa jeshi la Uganda linashirikiana na wanajeshi wa Sudan
kupambana na waasi nchi Sudan Kusini.
Mapigano hayo ambayo yalizuka mwezi uliopita
yanaendelea katika maeneo kadhaa ya Sudan kusini, licha ya kufufuliwa
kwa mazungumzo ya amani katika nchi jirani ya Ethiopia.Kwa mujibu wa msemaji wa jeshi, Luteni Kanali Paddy Ankunda, Uganda ina takriban wanajeshi elfu moja na mia sita nchini humo.
Serikali ya Uganda imekiri kukabiliana na waasi hao tangu mwanzoni mwa wiki hii,wakati wanajeshi hao waliposhambuliwa na waasi wanaoongozwa na makamu wa zamani wa Rais Riek Machar.
Akisimulia kuhusu tukio hilo kwenye mkutano wa kikanda nchini Angola mnamo Jumatano, Rais Yoweri Museveni, alisema kwamba baadhi ya wanajeshi wake waliuawa au kujeruhiwa.
Jeshi la Uganda hata hivyo halijaeleza idadi kamili ya wanajeshi waliouawa.
Luteni Kanali Paddy Ankunda ametetea hatua ya Uganda kupeleka wanajeshi wake Sudan Kusini ikisema lengo lake ni kulinda raia na kufungua njia kwa misaada kuingizwa nchini humo .
Na BBCSwahili