Rais Viktor Yanukovich amesema leo kuwa yuko tayari kukutana na marais watatu wa zamani wa Ukraine kujadili njia za kujitoa kutoka katika mzozo wa kisiasa ambao umeidhoofisha nchi hiyo. Mkuu wa sera za mambo ya kigeni wa Umoja wa Ulaya Catherine Ashton anaelekea Ukraine kusaidia kuutatua mzozo huo.
Akizungumza na waandamanaji kiongozi wa upinzani kutoka chama cha UDAR Vladimir Klitschko amewataka kuandamana kwa amani.
Mamia ya polisi wameingia katika eneo la kati la mjini Kiev leo wakati maandamano ya kupinga serikali yakiikumba Ukraine kwa wiki ya pili sasa, na kuzusha hofu ya hatua kali zitakazochukuliwa na serikali.
Rais Viktor Yanukovich amekumbana na wiki kadha za maandamano baada ya kukataa kutia saini makubaliano na Umoja wa Ulaya mwezi uliopita na kuamua kuhusiana na Urusi.
Polisi wamewekwa katika maeneo nje ya jengo la halmashauri ya mji wa Kiev, wakati ambapo waandamanaji nao wameweka vizuwizi katika baadhi ya mitaa .