Godane, ambaye pia anajulikana kama Mukhtar Abu al-Zubair, alitangaza kuwa al-Shabaab itategemea mbinu za vita vya msituni. "Ningependa kuwaambia taifa la Kiislamu na Wajahideni wake wasomi, hususani Mullah Omar na Shekhe Ayman al-Zawahiri […] kuwa jeshi hilo linaweza kuwa la Kijahidini nchini Somalia na kwamba wametikisa jihadi ya kiroho ambayo inategemea kushambulia na mapigano kuleta hali isiyo na utulivu kwa adui katika maeneo anayoyadhibiti," alisema.
Ujumbe wa Godane ulikuja siku mbili kabla ya wapiganaji wake kukimbia mji wa Jowhar, mji mkubwa kabisa uliokuwa umebakia chini ya udhibiti wao, wakati Askari kutoka Jeshi la Taifa la Somalia na Misheni ya Umoja wa Afrika Somalia walipokuwa wanaukaribia. Jowhar, mji mkuu wa mkoa wa Shabelle ya Kati, ni mmoja wa miji mikuu ya kanda uliotekwa na vikosi washirika wa serikali mwaka jana, ikiwa ni pamoja na Kismayu, Marka, Beledweyne, Baidoa na Hudur.
Kanali mstaafu Omar Mohamed, mshauri wa jeshi la Somalia, alisema tangazo la Godane kwamba kundi lake linaelekea katika vita vya msituni na mbinu za mashambulio ya kuvizia linaonyesha kuongezeka kwa udhaifu wa al-Shabaab.
"Ujumbe wa Godane unaonyesha kushindwa kabisa kutokana na kikundi kinavyopata mateso, pamoja na hali ya kukata tamaa ambayo inawahuzunisha wanachama wake wahalifu," aliiambia Sabahi. "Anachojaribu kufanya ni kuongeza hamasa ya wapiganaji wake waliokata tamaa."
"Kama tukiangalia muda wa ujumbe huu, unakuja wakati al-Shabaab iko katika kuzingirwa pande zote na inakumbana na upotezaji mkubwa siku hadi siku kutokana na mapigo makubwa ambayo wamekuwa wakikabiliana nayo kutoka kwa jeshi la taifa na washirika wake," alisema. "Wanachama wa wapiganaji wa al-Shabaab wanaishi katika hali ya kukata tamaa na udhaifu kwa kuwa hawawezi kukwepa kubanwa kwa nguvu na vikosi vya jeshi vya taifa."
Mohamed alisema wapiganaji wa al-Shabaab hawana uchaguzi mwingine wowote bali kuweka chini silaha zao na kujisalimisha kwa serikali. "Wanakimbia katika miji mikubwa na kupata hifadhi katika maeneo ya vijijini ambayo yako mbali sana na vikosi vya washirika, lakini hawawezi kupata mahali salama pa raha popote pale nchini."
habari na Sabahi Online