Waziri wa Uchumi wa Israel Naftali Benett amesema leo hii nchi hiyo inapanga kulishawishi bunge la Marekani kuzuwiya kufikiwa makubaliano kuhusu mpango wa nuklea wa Iran.
Naftali Benett |
Ameiambia radio ya jeshi kwamba kabla ya kuanza tena kwa mazungumzo hayo watawashawishi wabunge kadhaa wa Marekani ambao yeye mwenyewe binafsi atazungumza nao wakati wa ziara yake inayoanza Jumanne kwamba usalama wa Israel uko hatarini.
Benett alikuwa akizungumza baada ya Iran na mataifa yenye nguvu duniani kushindwa kufikia makubaliano kuhusu mpango wa nuklea wa Iran licha ya kuwa na mazungumzo ya siku tatu na kuvunja matumaini ya kufikiwa makubaliano yaliokuwa yakitafutwa kwa muda mrefu kuhusu mzozo huo wa muongo mzima.
Hata hivyo wanadiplomasia wanasema kwamba hatua kubwa za maendeleo zimefikiwa katika mazungumzo hayo na kwamba mazungumzo yataanza tena mjini Geneva tarehe 20 Novemba.