Waelimishaji wa Kenya watatizwa juu ya matokeo mabaya ya wanafunzi wa shule za umma

Waelimishaji wanatatizwa juu ya kuendelea kwa matokeo mabaya ya wanafunzi wa shule za umma kwenye mitihani ya taifa baada ya zaidi ya asilimia 50 ya wale waliofanya mtihani wa masomo ya Cheti cha Elimu ya Msingi cha Kenya (KCPE) mwaka jana kupata alama za chini ya wastani.

  • Wanafunzi wa Shule ya Msingi ya Gitwe katika wilaya ya Eldoret wakiwa wamekusanyika kwa ajili ya mkutano tarehe 26 Juni, 2009. [AFP]
    Wanafunzi wa Shule ya Msingi ya Gitwe katika wilaya ya Eldoret wakiwa wamekusanyika kwa ajili ya mkutano tarehe 26 Juni, 2009. [AFP]
"Mwelekeo huu unaleta wasiwasi na kutatiza akili. Kwani wengi wa watoto wanaosoma shule za umma wameendelea kupata alama mbaya, Inakuwa wazi zaidi kwamba mtoto atafanya vizuri kama atakwenda shule binafsin za akademia, ambazo wengi wa watoto maskini hawataweza kumudu," Katibu Mkuu wa Chama cha Wazazi cha Taifa la Kenya Musau Ndunda aliiambia Sabahi.
Kwa mujibu wa data zilizotolewa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia tarehe 31 Disemba, kati ya wanafunzi wa darasa la nane 839,759 ambao walifanya KCPE mwaka wa 2013, ambayo inatumika kama mtihani wa kuingia kidato cha kwanza, 467,353 walipata alama chini ya wastani, wakipata alama chini ya 250 kati ya 500.
Kati ya 467,353 ambao alama zao zilikuwa chini ya wastani, takribani 10,000 walipata chini ya 100 katika masomo matano yaliyofanyiwa mtihani, kwa mujibu wa wizara hiyo.
"Kinachoshangaza ni kwamba wengi wa wale waliopata alama za chini ya wastani ni watoto kutoka shule za umma, ambao wazazi wao hawawezi kumudu kuwapeleka shule binafsi," Ndunda alisema. "Kama mwelekeo huu hautabadilika kwa haraka, tutakuwa tukiwasukuma watoto wa kiume na kike wa maskini kushindwa."
Mpekethu Uniter Riziki, kutoka Shule ya Kulala ya Kathigiri huko Meru, ni mtahiniwa pekee kutoka shule za umma ambaye yumo miongoni mwa wanafunzi bora 100 kitaifa ambao waliopata zaidi ya alama 430. Mwanafunzi bora kabisa katika mtihani huo alipata alama 444. Riziki alipata alama 442.
Ndunda aliwalaumu walimu kwa matokeo mabaya, akiwatuhumu kwa kutotimiza kikamilifu majukumu yao.
"Kushughulikia hili, wizara ya elimu inapaswa kuwa na kozi ya lazima ya msasa kwa walimu wote, pamoja na wakuu wote wa shule kusaini mikataba ya matokeo," alisema.
Ndunda alisema hatua za kinidhamu zinapaswa kuzingatiwa dhidi ya walimu ambao wanafunzi wao wanaendelea kufanya vibaya katika mitihani ya taifa.
"Hatua za kinidhamu zijumuishe kushushwa cheo, kukatwa mshahara, na kuhamishwa kwa wale walimu watakaoshindwa kutoa matoke yanayofaa," alisema.
Matokeo mabaya katika mtihani wa hivi karibuni yalithibitisha utafiti wa Uwezo Kenya, jitihada ya miaka minne kuboresha lugha na ujuzi wa hesabu miongoni mwa watoto wenye umri wa miaka 6 hadi 16 nchini Kenya.
"Mwaka 2012 utafiti wetu yalionyesha maendeleo kidogo katika uwezo wa kujifunza wa watoto," alisema John Mugo, Mratibu wa Nchi ya Kenya wa Uwezo
"Haiko mbali na ripoti zetu, ambazo zilionyesha kwamba wanafunzi wa darasa la nane hawawezi kufanya hesabu rahisi za darasa la pili, pamoja na kuzungumza na kuandika kwa usahihi Kiingereza na Kiswahili, ujuzi uliopatikana katika elimu ya awali ya msingi, kulikuwa na kuonyeshwa kwa matokeo mabaya katika hesabu na lugha katika mitihani ya KCPE ya 2013" Mugo aliiambia Sabahi.
"Viwango vya mafunzo vinapungua, pamoja na viashirio dhahiri vya [matokeo] mabaya katika shule zote za umma," aliendelea kusema. "Matokeo yetu na mtihani wa mwaka huu yameonyesha kwamba watoto na hususani [wale] wanaotoka katika shule za umma hawapati stadi za msingi katika kusoma na kuandika na katika hesabu."
"Walimu walio wengi katika shule za umma wanachagua kutokwenda shuleni, na kuwashangaza wale wanaoingia madarasani [hawatekelezi majukumu yao] wanapofundisha," Mugo alisema. "Matokeo yake hili limeathiri uwezo wa kujifunza wa wanafunzi kwa kuwa wanapata muda mdogo wa kukamilisha mitaala".
Mugo alitoa wito wa mchakato wa ufuatilia na tathmini kwa makini ambao utawahamasisha walimu kufundisha kutokana na mitaala, na kuwaomba wazazi wa wanafunzi wa shule za umma kujihusisha katika maendeleo ya watoto wao.

Wanafunzi wengi sana, hakuna walimu wa kutosha

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Chama cha Taifa cha Walimu Kenya (KNUT) Wilson Sossion amewaondolea walimu lawama, akisema kwamba madarasa yaliyojaa sana ndiyo tatizo.
Akikiri kwamba ilikuwa usumbufu kuwa wanafunzi wengi walifeli mitihani na wanaweza wasiende shule za sekondari, Sossion alisema serikali ilaumiwe kwa kutoongeza idadi ya walimu katika shule za umma.
Tangu kuanzishwa kwa elimu ya msingi ya bure mwaka 2002, idadi ya wanafunzi wanaojiunga na shule imeongezeka, wakati ambapo idadi ya walimu imebakia ile ile, Sossion alisema.
"Ni makosa kuwalaumu walimu kwa waliofeli [wakati] serikali imekataa kuajiri walimu zaidi ili kuoanisha kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi," alisema.
Aliongeza kwamba serikali imeshindwa kugharimia kikamilifu sekta ya elimu ya umma.
"[Ugharimiaji] wa serikali kwa kila mwanafunzi umekuwa hautoshi na hii ni moja ya mambo ya msingi ambayo yanashusha matokeo ya shule za umma."
Licha ya kuajiri walimu zaidi na kuongeza ugharimiaji wa shule za umma, Sossion alisema kuna haja ya kuwapa motisha walimu kwa kuwalipa vizuri.
Waziri wa Elimu Jacob Kaimenyi alisema kwamba licha ya matokeo ya wanafunzi katika mitihani, shule za umma kwa ujumla zimeimarika katika matokeo ya jumla.
Kati ya shule 20 za kwanza zilizoimarika vizuri, 18 zilikuwa shule za umma, alisema.
"Kwa ujumla mwaka 2013 ulikuwa mwaka mgumu kwa shule za umma," aliiambia Sabahi, akieleza kwamba kufungwa kwa shule za umma wakati wa uchaguzi mkuu wa 2013 na mgomo wa walimu wa mwezi mmoja wa Julai vingekuwa na athari kubwa kwa matokeo ya wanafunzi.
"Kwa wakati huu hatuwezi kulaumu matokeo hayo mabaya katika jambo lolote," alisema, akiongeza kwamba wizara itafanya mkutano wa wadau mwezi ujao ili kutathmini mambo yote yanayochangia.
Wakati huo huo, Kaimenyi alisema serikali imeanzisha kozi ya ustadi ya walimu ambayo inadhamiria kuongeza ubora na matokeo ya shule kwa kuwataka walimu kuhudhuria kozi ya kupiga msasa na kupimwa katika umahiri wao.
Pia serikali katika wiki tatu zijazo itatekeleza ujumuishaji wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano katika [shule] za msingi ambapo tutatoa kwa wanafunzi wote wanaojiunga na shule za msingi za [umma] kompyuta ya mkononi ambayo itatumika kama chombo cha marekebisho ya mtaala ambacho kitabadilisha matokeo ya shule," alisema.
Utekelezaji wa programu ya kompyuta za mkononi ijulikanayo kama laptop, kulipiwa na fedha zilizokusudiwa kwa ajili ya duru ya pili ya uchaguzi wa urais mwaka 2013, utatimiza moja ya ahadi za Rais Uhuru Kenyatta kwa siku zake100 madarakani.
Kaimenyi alieleza kwamba mradi wa kompyuta za mkononi utaongeza ari ya wanafunzi katika kujifunza, na kufanya kuwa rahisi kwao kuelewa masomo magumu.