Deo Filikunjombe ni nani?


Deo Filikunjombe ni nani? Deo Haule Filikunjombe alikuwa Mbunge wa jimbo la ludewa, mkoani Njombe kuanzia mwaka 2010 na alikuwa akigombea kwa muhula wa pili kabla ya kifo chake juzi. Alizaliwa Machi 4, 1972 na akaanza darasa la kwanza katika Shule ya Msingi ludewa mwaka 1986 na akaingia Kasila Seminari kuanzia mwaka 1989- 1992, baadaye akajiunga na Sekondari ya Forest Morogoro 1994- 1996. Filikunjombe alijiunga na Chuo Kikuu cha Makerere, Uganda mwaka 1996-1999 ambapo alitunukiwa shahada ya kwanza (BA), akiwa huko aliitumikia Redio One Stereo kama mwakilishi wa kujitegemea (Correspondent). Baadaye alijiunga na Chuo cha Diplomasia kilichopo Dar es Salaam mwaka 2001-2002 ambapo alisomea lugha na akapata cheti. Mwaka 2000- 2001 alijiunga na Chuo cha Polisi (CCP) Moshi ambako alitunukiwa cheti. Mwaka 2002 -2005 alifanya kazi World Vision international Tanzania akiwa ni Meneja wa Mawasiliano ya Umma. Katika uchaguzi wa mwaka 2000 alikuwa mmoja wa waangalizi wa uchaguzi, akihusika zaidi na vyombo vya habari (Media Monitor).
 
Aliwahi kufanya kazi katika Gazeti la The New Vision  mwaka 1998 hadi 1999 kama mpiga picha wa kujitegemea. Na Wakati anasoma Chuo Kikuu cha Makerere aliteuliwa kuwa Meneja wa Mawasiliano chuoni hapo.

Hapa nchini aliwahi kufanya kazi katika Gazeti la The Guardian  kama mwandishi wa kolamu mbalimbali (columnist). Kazi zake kichama, licha ya kuwa mbunge, aliteuliwa kuwa kamanda wa vijana wilayani Njombe kuanzia mwaka 2009  na bungeni alikuwa  Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali na Mashirika ya Umma, kazi ambayo aliifanya kwa umakini mkubwa. Filikunjombe akiwa bungeni aliwahi kutoa tuhuma kwamba viongozi wakuu wa Bunge kwamba walikuwa wakati fulani, wakiingilia utendaji kazi wa kamati hiyo muhimu siyo tu kwa bunge bali pia kwa taifa kwa ujumla. Kamati hiyo ilikuwa muhimu kwa kuwa alisema ilipaswa kufanya kazi zake kwa niaba ya Watanzania wote, japo kwa kupitia ‘muhuri’ wa Bunge. “Kwa upande wetu hatutaki kuwamo katika orodha ya watakaothibitisha tuhuma kwamba spika na naibu wake wamekuwa wakiingilia utendaji wa kamati hiyo. Hata hivyo, tunaamini kama hivyo ndivyo hali ilivyo au hata kama hali haiko hivyo, ni busara zaidi kwa viongozi hao wakuu wa Bunge ama kujirudi au kuendelea kubaki katika mwenendo sahihi wa kiuongozi, na hasa ikizingatiwa msemo mashuhuri kwamba, lisemwalo lipo, kama halipo laja,” hayo yalikuwa maneno mazito ya Filikunjombe bungeni enzi za uhai wake.