Aliyekuwa kada wa Chadema Ikungi, Singida, Hamisi Mazonge, arejea CCM na kukiomba radhi


DSC01397
Aliyekuwa katibu mwenezi CHADEMA kata ya Ikungi mkoani Singida, Hamisi Yahaya Mazonge, akitangaza uamuzi wake wa kuhama CHADEMA na kurejea CCM,  kwenye mkutano wa uzinduzi wa kampeni za uchaguzi nafasi ya ubunge na udiwani jimbo la Singida mashariki.Mazonge amedai kwamba amehama CHADEMA baada ya kubaini chama hicho hakina sera yoyote ya kuwaletea wananchi maendeleo.(Picha naNathaniel Limu).
Na Nathaniel Limu, Ikungi
ALIYEKUWA Katibu mwenezi wa CHADEMA Kata ya Ikungi wilaya ya Ikungi mkoani Singida, Hamisi Yahaya Mazonge, amerejea CCM na kukiomba radhi Chama chake hicho, kwa madai amekifanyia kosa kubwa wakati akiwa CHADEMA.
Mazonge alitaja kosa hilo kuwa ni kukinyang’anya Chama cha Mapinduzi (CCM), vijiji vya Ikungi,Ighuka, Mbwajiki na Matongo kwenye Uchaguzi wa serikali za mitaa na kuwa chini ya mikono ya CHADEMA.
Alisema anajutia kosa hilo la kusababisha vijiji hivyo vinne vilivyokuwa chini ya CCM kwa miaka mingi, kuhamia CHADEMA. Amedai pia kipindi hicho alitumia nguvu kubwa kuchangia pia vitongoji 11 kati ya vitongoji 22 vya kata ya Ikungi,kuhamia CHADEMA.
“Wana CCM wenzangu,kutoka chini ya sakafu ya moyo wangu,najutia sana kufanya kosa hili ambalo kwa vyo vyote,litakuwa limeathiri kwa kiasi kikubwa ustawi wa CCM katika kata yetu”,alisema.
Mazonge ambaye ameonyesha dhahiri kujutia kosa hilo,amekiomba radhi Chama Cha Mapinduzi wakati akizungumza kwenye mkutano wa uzinduzi wa kampeni za ubunge na udiwani katika jimbo la Singida mashariki uliofanyika katika makao makuu ya wilaya ya Ikungi mkoani Singida.
Aidha,alisema amefikia uamuzi wa kurejea CCM baada ya kubaini CHADEMA jimbo la Singida mashariki kwa miaka mitano iliyopita, imedumaza kwa kiwango kikubwa  maendeleo ya jimbo hilo.
Mazonge ameahidi kuwa kuanzia sasa atakuwa mwanachama mwaminifu wa CCM na atatumia nguvu za ziada, kuhakikisha vijiji na vitongoji hivyo vinarejea mikononi mwa CCM.
Naye Mkulima na mfugaji wa kijiji cha Ng’ogousoro Kata ya Isuna, Chapa Chapa Elias, amesema amerejea CCM baada ya kutokufurahishwa na kitendo cha CHADEMA,kupokea  makapi kutoka CCM na kuyauzia chama kizima kizima.
“Binafsi kwa sasa CHADEMA chama ambacho kilianza kwa na nguvu ya upinzani ya kweli, kimebadilika ghafla na kuwa kama choo ambacho kazi yake ni kupokea kila aina ya taka taka. Kwa ujumla kwa sasa CHADEMA hakieleweki kabisa”,alisema Chapa kwa masikitiko.
Kwa upande wake Mchungaji wa Kanisa la Pentekoste kijiji cha Ikio Ponisian Ghumpi, amehama CHADEMA kwa madai kwamba kwa sasa chama hico hakina dhamira ya kweli ya kuwatumikia wananchi.
Kama hiyo haitoshi,mjumbe wa halmashauri kuu ya taifa (NEC) ya CCM kutoka Rombo, Evod Mmanda, ambaye alikuwa kwenye msafara wa kampeni ya mgombea mwenza wa urais,alitumia nafasi hiyo,kumwanika Tundu Lissu,hadharani na kumwacha akiwa ‘mtupu’.
Mmanda alisema anamfahamu vyema Lissu na kwamba uwezo wake wa kuongoza ni mdogo, hivyo kuendelea kumchagua kuwa Mbunge ni sawa na kutafuta matatizo.
“Wana Singida Mashariki tokeni kwenye mchepuko (CHADEMA) na kusema kufanya kosa si kosa, lakini mimi nasema mlifanya kosa kumchagua Tundu Lissu”,alisisitiza.
Kuhusu mgombe wa CCM Jonathan Njau,alisema;“Namfahamu Njau miaka 15, ni mtu mwelewa na mpenda maendeleo. Tundu Lissu namfahamu tangu akiwa kidato cha nne, ni mtu msanii na mhamasishaji wa fujo, kamwe ndugu zangu wa Singida msifanye makosa ya kumrejesha madarakani tena”. Alisema.
Mmanda alisema Lissu amekuwa akihamasisha wananchi wasishiriki katika shughuli za maendeleo kama vile kuchangia miradi ya elimu na afya, jambo ambalo limesababisha jimbo hilo, kuwa nyuma kimaendeleo.
“Wana Ikungi mnahitaji madaktari, wahandisi na wataalamu wa kilimo na mifugo kwa vile ninyi mnajishughulisha na mambo haya. Sasa kama mtu anakataa kuchangia maendeleo, anataka mkose madaktari na wanasayansi ili muendelee kuwa masikini. Hakika mtu huyu anayeitwa Tundu Lissu, si mzuri na hapaswi kuchaguliwa kabisa,” alisema.
Aliongeza: “Tundu Lissu hana nia ya dhati ya kuwaendeleza wana Singida mashariki. Mfano mzuri ni kwamba watoto wake na wa mdogo wake wanasoma Zanzibar kwenye shule ambazo zina maabara zilizokamilika”.