Dk Shein : lazima tuwe na mpango maalum kuzifanyia matengenezo barabara zinapoharibika


STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
    Zanzibar                                                                   26 Agosti , 2015
---
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano pamoja na Mfuko wa Barabara wametakiwa kuhakikisha kuwa wanakuwa na mpango maalum wa kuzifanyia matengenezo barabara nchini ili barabara hizo ziweze kudumu kwa muda mrefu.

Akizungumza mara baada ya kuzindua rasmi barabara za Wete-Gando na Wete Konde jana Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein alisema kumekuwa na ulegevu katika kuzifanyia matengenezo barabara na matokeo yake ni barabara hizo huachwa hadi kufikia hali ya kuharibika kabisa.

Katika hafla hiyo iliyofanyika huko katika kijiji cha Ukunjwi, wilaya ya Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba, Dk. Shein alibainisha kuwa azma ya serikali ni kuhakikisha kuwa kisiwa cha Pemba sasa kinaunganishwa kwa barabara kila upande kama ilivyo kwa kisiwa cha Unguja hivyo serikali imo mbioni kutekeleza mradi wa ujenzi wa barabara ya Ole hadi Kengeja (35 km) ambayo ilibuniwa na Rais wa Kwanza wa Zanzibar Mzee Abeid Amani Karume.

Alieleza pamoja na barabara hiyo, serikali inaifanyia marekebisho makubwa barabara ya Ole hadi Konde ambayo ni ya kiwango cha lami kuimarisha uwezo wake na pia barabara ya zamani kutoka Chake-Chake hadi Wete (22.1 km) ujenzi wake utaanza hivi karibuni kupitia fedha za mkopo wa Benki ya Kiarabu  ya Maendeleo ya Uchumi ya Afrika (BADEA) na Mfuko wa Maendeleo wa Saudi Arabia(Saud Fund).

Dk. Shein alitoa wito kwa wananchi kuzitunza barabara hizo kwa kuepuka vitendo vinavyopelekea kuharibu barabara ikiwemo uchimbaji wa mchanga na mawe maeneo ya barabara pamoja na kutoondoa alama za barabarani yakiwemo mabango mbalimbali yanayoelekeza watumiaji wa barabara hizo.
Kuhusu kukamilika kwa ujenzi wa barabara za Wete- Gando na Wete- Konde 

Dk. Shein aliwapa changamoto wananchi kwa kuwataka kuzitumia barabara hizo kujiimarisha kiuchumi kwa kupanua shughuli zao za uzalishaji mali ikiwemo kilimo cha matunda na mbogamboga.