Na Mwandishi Wetu Pemba.
MakamuMwenyekiti wa CCM Zanzibar na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amemuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungao Dk. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuwathibitishia wananchi na wanaCCM kuondoa shaka na hofu kwani Serikali yao ipo na itaendelea kuwalinda siku ya uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Dk. Shein ambaye ni Mgombea nafasi ya Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM aliyasema hayo katika hotuba yake aliyoitoa kwenye mkutano wa kufunga Kampeni ya chama hicho uliofanyika huko katika viwanja vya Gombani ya Kale, Chake Chake, Pemba uliohudhuriwa na maelfu ya wananchi na wanaCCM.
Dk. Shein alitoa shukurani kwa wanaCCM na wananchi kwa kuhudhuria kwa wingi katika mikutano yote tokea tarehe 13 mwezi huu zilipozinduliwa Kampeni za chama hicho.
Alisema kuwa katika mikutano hiyo ahadi kwa kila Jimbo, Wilaya hadi Wadi zilitolewa kwa mujibu wa utekelezaji wa Ilani ya CCM pamoja na kuelezea mambo makubwa kwa Zanzibar.
Alisema kuwa katika miaka mitano ijayo baada ya kuchaguliwa yeye na chama chake atayatekeleza yale yote yalioahidiwa na chama chake.
Dk. Shein aliahidi kutokana na Ilani ya chama hicho kuendeleza kusimamia amani, utulivu na umoja kwani ndio njia pekee ya kuleta maendeleo.
"Anaezania ni zihaka na anataka kufanya fujo ajaribu aone",alisema Dk. Shein.