Moja ya eneo lililoaribika kutokana na hali ya mabadiliko ya tabianchi (Climate Change) katika fukwe ya Kilindoni, katika Kisiwa cha Mafia, Mkoani Pwani, nchini Tanzania. (Picha zote na Andrew Chale, Modewjiblog).
Afisa Mazingira wa Wilaya ya Mafia, Bw. Gideon Zakayo.
Na Andrew Chale, Modewjiblog
[MAFIA-ISLAND] Kisiwa cha Mafia kijografia kipo karibu na mlango wa Mto Rufiji kusini mwa Tanzania.
Hata hivyo, Kisiwa hichi ambacho ni Wilaya moja wapo ya Mkoa wa Pwani inakabiriwa kwa kiwango kikubwa na changamoto za Mabadiliko ya tabianchi hasa baada ya wananchi wake wengi kutopata elimu hiyo sahihi.
Imeelezwa kuwa, elimu juu ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi katika Kisiwa cha Mafia ambacho pia kinaunda visiwa vidogovidogo zaidi ya vitano, wananchi walio wengi katika kisiwa hicho bado hawajapata elimu sahihi ya kukabiliana na mabadiliko ya kimazingira (Climate Change).
Mtandao huu ambao ulipiga hodi katika kisiwa hicho cha Mafia ili kupata habari za mabadiliko ya tabianchi na namna ya Mabadiliko ya tabianchi yanavyo athiri Kisiwa hicho (How Climate Change effects Mafia Island in Tanzania) ambapo iliweza kuzungumza na maafisa Ardhi, Mazingira na wananchi wa Wilaya hiyo, na kueleza haya:
Kwa upande wa Afisa Mazingira wa Wilaya hiyo, Gideon Zakayo (pichani juu) amebainisha kuwa, Kisiwa cha Mafia kinakabiliwa na changamoto mbalimbali za Kimazingira ikiwemo hali ya Mabadiliko ya tabianchi huku suala la elimu kwa wananchi likiwa dogo kutokana na kutokuwa na fungu la kutosha.
“Kwa sasa bado hatuna fungu la kutosha kuwafikia wananchi na kutoa elimu ya Mabadiliko ya tabianchi. Ila bado milango ipo wazi kwa mashirika na taasisi binafsi kufika na kutoa elimu hiyo kwa sasa” anasema Zakayo.
Zakayo ameongeza kuwa, Suala la Mazingira ni pana kwani limejumuisha Afya, Maji, Kilimo, Misitu, ardhi na mazingira yote kwa ujumla hivyo wadau wanahitajika kujitokeza kusaidiana na Serikali katika kutoa elimu, kuelimisha sera na taratibu zinazotakiwa kufuatwa na wananchi katika maeneo husika.
Aidha, ameongeza kuwa, katika miongoni mwa visiwa vidogo vidogo ndani ya Mafia, kuna baadhi ya visiwa vimeanza kuharibiwa kutokana na Mabadiliko ya tabianchi.
“Vipo visiwa baadhi tayari vimeanza kuathirika na mabadiliko hayo kwani maji yamekula ardhi. Pia baadhi ya maeneo maji yameweza kuingia katika ardhi na kubadilisha maeneo hayo tofauti na awali.” amebainisha Zakayo, Afisa Ardhi Wilaya ya Mafia.