Kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga amemsamehe mzee aliyempiga bakora katika mkutano wa hadhara wa kisiasa katika jimbo la Kwale Pwani ya Kenya,
Mwanamume huyo, Lengo Mdzombo, anayefanya kibarua katika shamba moja Kwale, alikamatwa Jumanne na kufikishwa mahakamani.
Alishitakiwa kwa kosa la kumshambulia kiongozi huyo pamoja na gavana wa Kwale.
Hali ya taharuki ilitanda katika mkutano wa hadhara Jumatatu wiki hii baada ya Mdzombo kwenda ukumbini na kuanza kumtandika bakora kiongozi wa upinzani Raila Odinga pamoja na wanasiasa wengine.
Raila alikuwa amejiunga na kikundi cha wanawake waliokuwa wanacheza densi ya kitamaduni kuwatumbuiza wageni, pamoja na gavana wa jimbo la Kwale Pwani ya Kenya Salim Mvuruya katika mkutanmo wa kisiasa.
Raila alikuwa ameambatana na viongozi wengine, wakiwemo, Seneta Juma Boy, Hassan Omar, Agnes Zani, James Orengo, Johnstone Muthama na wengineo.
Mzee huyo alimpiga bakora Odinga ambaye ni waziri mkuu wa zamani kabla ya kumgeukia gavana wa jimbo hilo na kumchapa mara mbili. Hata hivyo mwanamume huyo alishindwa nguvu na walinzi wa Raila Odinga.
Polisi walithibitisha kuwa walimkamata mwanamume huyo na kumwachilia baada ya kugundua kuwa alikuwa na matatizo ya kiakili.
Haijulikani kwa nini mwanamume huyo alimshambulia Raila ila baadhi wanasema ni kwa sababu alighadhabishwa pale waziri mkuu alipocheza densi na mwanamke aliyesemekana kuwa mke wake ambaye alikuwa katika kikundi cha wanawake waliokuwa wanawatumbuiza wageni waheshimiwa.
Viongozi waliofika walilazimika kusitisha densi hiyo kabla ya mwanamume huyo kushindwa nguvu.