Januari 20, 2014
Kamati ya Ujenzi Mpya ya jengo la maduka la Westgate nchini Kenya ilianza vikao vyake vya wazi kwenye ukumbi wa Charter Hall jijini Nairobi siku ya Jumatatu (tarehe 20 Januari), kiliripoti kituo cha Capital FM cha Kenya.
Kamati hiyo imepewa jukumu la kusimamia ujenzi mpya wa jengo la Westgate katika namna ambayo inapunguza hasara ya kupotea kwa ajira na gharama nyenginezo za kifedha.
Yale yatakayosemwa na umma katika vikao hivyo vya wiki moja yatajumuishwa kwenye ripoti ya kamati hiyo juu ya mapendekezo yake ya ujenzi mpya.
"Kama kamati, tunajitahidi kutayarisha ripoti yenye ushauri wa kina kuwezesha mkakati wa ujenzi mpya ambao unajumuisha wote kwa ajili ya jengo la Westgate huku tukizingatia mpango wa taifa wa kujibana kiuchumi tunapokabiliana na mikasa kama hii ya kusikitisha," alisema makamu mwenyekiti wa kamati hiyo, Wahame Muchiri.