Mgomo Kenya; Walimu Waigomea Mahakama…!


Moja ya madarasa yakiwa tupu kutokana na mgomo wa walimu unaoendelea nchini Kenya.
Moja ya madarasa yakiwa tupu kutokana na mgomo wa walimu unaoendelea nchini Kenya.

UFUNDISHAJI masomo anuai katika shule za umma nchini Kenya umekwama licha ya amri ya mahakama ya kuwataka walimu ikilazimisha warejee shuleni Jumatatu. Mgomo wa walimu nchini Kenya umeingia wiki ya tano hivi sasa huku ufundishaji ukiendelea kuathirika.
Vyama vya walimu nchini Kenya vimesema havitatekeleza amri ya mahakama iliyowataka kusitisha mgomo huo kwa siku tisini kuanzia leo. Badala yake vyama hivyo vimerejea mahakamani leo kutaka ufafanuzi zaidi kuhusu uamuzi huo.
Hata hivyo kesi yao iliahirishwa hadi alhamisi wiki hii. Walimu walijitokeza kwa wingi wakiandamana na viongozi wao wa vyama vya walimu mwendo wa saa nane unusu. Walimu walikwenda mahakamani kutafuta ufafanuzi kuhusu ratiba ya mihula ambayo serikali ilibadilisha hapo awali mgomo ulipochacha.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi siku ya Alhamisi saa nane u nusu kwa sababu jaji aliyekuwa akisikiza kesi hiyo aliomba radhi iliapokee matibabu. Jijini Nairobi hii leo shule ya Msingi ya Moi Avenue na Shule ya Msingi ya Nairobi hazikuwa na wanafunzi. Wanafunzi wamesalia nyumbani huku walimu wakiwa wamegoma kurejea shuleni kama walivyoagizwa na mahakama ya nchi hiyo.
-BBC