Mabadiliko sasa kuhamia CCM, bungeni
Rais Jakaya Kikwete akimuapisha Jenister
Mhagama kuwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi katika hafla
iliyofanyika katika Viwanja vya Ikulu, jijini Dar es Salaam jana. Picha na
Emmanuel Herman
Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Bunge la Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, vitalazimika kufanya mabadiliko katika safu zake za
uongozi kutokana na athari zilizosababishwa na mabadiliko yaliyofanywa na Rais
Jakaya Kikwete katika Baraza la Mawaziri.
Juzi, Ikulu ilitangaza mabadiliko katika
baraza hilo ambayo yaliwaweka kando mawaziri na manaibu waziri watano, huku
sura kumi mpya zikiingia, mabadiliko ambayo yameacha nafasi mbili wazi katika
sekretarieti ya CCM na nafasi nne katika uongozi wa Bunge.
Miongoni mwa walioteuliwa na kuapishwa jana
ni waliokuwa wajumbe wa Sekretarieti ya CCM; Dk Asha-Rose Migiro ambaye
ameteuliwa kuwa Waziri wa Katiba na Sheria na Mwigulu Nchemba ambaye ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Fedha.
Nchemba ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM Tanzania
Bara, wakati Dk Migiro ni Katibu wa Halmashauri Kuu ya chama hicho, Siasa na
Uhusiano wa Kimataifa.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape
Nauye alisema jana kuwa viongozi wa sekretarieti ya CCM wanapoteuliwa kushika
nafasi nyingine za Serikali, wanalazimika kuziacha nyadhifa zao katika chama.
Nape alisema kwa maana hiyo, Mwenyekiti wa
CCM, Rais Kikwete atalazimika kuteua watu wa kuziba nafasi za Dk Migiro na
Nchemba. “Huu ni utaratibu tuliojiwekea katika chama kwamba viongozi wa
sekretarieti hawatafanya kazi mbili za chama na Serikali, kwa hiyo viongozi
hawa pia wataziacha nafasi za chama,” alisema Nape.
Hata hivyo Nape alisema utaratibu huo
hauwagusi wenyeviti wa chama hicho wa mikoa, ambao wameteuliwa kuwa mawaziri
ama manaibu waziri kwani uenyekiti si nafasi ya utendaji.
Katika uteuzi huo, Mwenyekiti wa CCM, mkoa
wa Simiyu, Dk Titus Kamani aliteuliwa kuwa Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na
Uvuvi, wakati Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya, Godfrey Zambi aliteuliwa kuwa
Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika.
“Hawa wanaweza kuendelea na nyadhifa zao za
uenyeviti katika chama, huku wakiwa na nyadhifa serikalini, hii haina athari
kwa sababu siyo watendaji wakuu wa chama,” alisema Nape.
Bungeni
Bunge pia litalazimika kuchukua hatua za
kuziba nafasi zilizoachwa wazi na
aliyekuwa Mwenyekiti wa Bunge pia Kiongozi wa Kamati ya Maendeleo ya Jamii,
Jenister Mhagama ambaye ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya
Ufundi.
Wengine ni Mahmoud Mgimwa aliyekuwa
Mwenyekiti wa Kamati ya Uchumi, Viwanda na Biashara na sasa ameteuliwa kuwa
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii na aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya
Katiba, Sheria na Utawala, Pindi Chana ambaye sasa ni Naibu Waziri wa Maendeleo
ya Jamii, Jinsia na Watoto.
Na MWANANCHI