Dhahabu' nyeusi yazizima Kenya


Kupatikana kwa mafuta Kenya kunaimarisha matumaini ya uchumi kunawiri
Kampuni ya kuchimba mafuta ya Tullow imetangaza kupata visima vipya vya mafuta katika jimbo la Turkana, Kaskazini mwa Kenya na kuinua matumaini ya uchumi wa Kenya kuimarika zaidi.
Kampuni hiyo ya Uingereza ambayo huendesha shughuli zake nyingi Afrika, imesema kuwa visima vyote vya mafuta vilivyogunduliwa katika eneo hilo lote tangu mwaka jana, vina uwezo wa kuzalisha mapipa milioni 600 .
Lakini imeongeza kuwa inaamini uwezo wa visima hivyo ambao utatathminiwa zaidi katika miaka miwili ijayo, unaweza kuwa zaidi ya mapipa bilioni moja.
Ugunduzi huu unafikisha saba visima vya mafuta vilivyogunduliwa na kampuni ya Tullow Kaskazini mwa Kenya.
Tullow inasema kuwa imekubaliana na serikali ya Kenya kuanza utafiti zaidi na kuona njia za kuweza kutengeza mabomba ya kusafirisha nje mafuta hayo.
Serikali ya Kenya inatarajia kuwa ifikapo mwaka 2015/16 itaanza rasmi kuuza mafuta yake.
Uganda na Kenya zimetangaza kufanya miradi ya pamoja ya kuwa na bomba la mafuta kuelekea bahari hindi.
Kampuni ya Tullow ilikuja kujulikana wakati ilipogundua mafuta nchini Ghana na Uganda.
Ugunduzi wa mafuta katika jimbo la Turkana umewachangamsha watu wengi nchini Kenya, lakini hata ikiwa mafuta hayo yatakuwa na thamani bado changamoto nyingi zinaisubiri Kenya.
Na BBCSwahili