UWANJA
wa kisasa unaojengwa kwa ajili ya michezo Wilayani Chunya mkoani hapa, umeibua
hisia tofauti kwa wananchi ambao wamekuwa wakihoji hati miliki ya
eneo la ujenzi huo.
Imedaiwa
kuwa kuna wasiwasi wa hapo baadae kukaibuka mkanganyiko ambao unahitaji ufafanuzi
mapema ili kuepusha manung’uniko kwa wadau wanaoendelea kuchangia ujenzi huo.
Akizungumza
na NIPASHE, Edward Hezron mkazi wa Kibaoni, alitoa mfano kwa uwanja wa Sokoine
wa Mbeya ambao umetajwa kwamba ujenzi wake ulitegemea michango na nguvu kazi ya
wananchi sambamba na michango ya watumishi wa Serikali lakini matokeo
yake CCM imekuwa ikikusanya mapato badala ya Serikali.
“Hofu
yetu ni inatokana na hatimiliki ya eneo la ujenzi wa uwanja huo, haitaleta
picha nzuri kama uwanja huo mapato yake yatakusanywa na Chama Cha Mapinduzi
kama ilivyo kwenye uwanja wa Sokoine ambao ulijengwa kwa michango ya watumishi
wa Serikali na nguvu kazi ya wananchi’. Alisema
Alisema
kuwa inasemekana kuwa uwanja wa Sokoine ulijengwa mwaka 1976 na kuzinduliwa
rasmi mwaka 1977, mafanikio yake yalitokana na michango ya wananchi kama ilivyo
kwa uwanja wa Chunya. Awali kabla ya uwanja wa Sokoine shughuli za michezo na
maonesho ya biashara zilikuwa zikifanyika kwenye viwanja vya Sabasaba vya
jijini Mbeya
Mwenyekiti
wa kamati ya ujenzi wa uwanja wa Chunya, Aidan Msigwa alisema kuwa ujio wa
uwanja huo unaotegemea kutumia zaidi ya Shilingi Bilioni 8, unatokana na wazo
la Mkuu wa Wilaya hiyo Deogratius Kinawiro ili kukuza vipaji na ajira ya
michezo kwa vijana
Msigwa
akizungumzia kuhusu hatimiliki alisema kuwa yeye anachojua uwanja huo ni mali
ya wananchi wa Chunya na Halmashauri ya Wilaya ni msimamizi kwa mujibu wa
kanuni za Serikali, na wananchi walitangaziwa wajitolee michango ili
kufanikisha ujenzi huo bila kujali itikadi zao za kisiasa
‘Ujio
wa uwanja huo ni wazo la Mkuu wa Wilaya kwa ajili ya watu wa Chunya na ndiyo
sababu waliweza kutangaziwa mapema wajitolee kuchangia ujenzi huku wakiziweka
kando tofauti zao za kisiasa, Halmashauri ni msimamizi kama ilivyo kwenye
vyanzo vingine vya mapato’. Alisema Msigwa
Hata
hivyo, vyanzo vingine vya habari vimefafanua kwamba mfumo wa chama kimoja cha
siasa kwa kipindi kile ndio uliokipa madaraka Chama Cha Mapinduzi kutawala
viwanja mbalimbali kitendo ambacho kwa sasa hakiwezi kutokea kwa sababu ya
mfumo wa vyama vingi vya siasa.