MFANYABIASHARA wa kubadirisha fedha za kigeni
mkazi wa Sogea katika mji mdogo wa Tunduma wilayani Momba mkoa wa Mbeya,
Alphonce Mwanjela amenusulika kifo baada ya kupolwa fedha na kisha kupigwa
risasi mguuni.
Akizungumza na waandishi wa habari mkoani
Mbeya, Kaimu Kamanda wa polisi Mkoa wa Mbeya Barakael Masaki, alisema kuwa mfanyabiashara
huyo alivamiwa nyumbani kwake na watu wanne wasio fahamika.
Alisema watu hao kabla ya kumpora walimjeruhi
kwa mapanga mfanyabiashara huyo na kisha kumpiga na risasi mguuni kwa kutumia
bunduki aina ya Short Gun.
Masaki alisema kuwa Mwanjela alipolwa fedha
za kitanzania Tsh. 5,200,000, Dola za kimarekani, Usd 2,300, Rand 10,000, na
fedha za Zambia Kwacha 2,000,000.
Alisema watuhumiwa hao walimvamia
mfanyabiashara huyo wakiwa umbali wa mita 50 kutoka nyumbani kwake.
“Mfanyabiashara huyu alivamiwa mita 50 kutoka
nyumba yake ilipo na alikuwa anatokea kufanya shughuli zake za kubadilisha
Fedha mpakani Tunduma,” Alisema Masaki.
Masaki ametoa wito kwa wafanyabiashara
wanaofanya biashara za aina hiyo kuto tembea na fedha kwani ni hatari.
Jeshi la Polisi linaendelea na kufanya
uchunguzi ili kuwabaini wahusina wa tukio hilo la uporaji wa kutumia risasi.