Utawala wa Shabelle ya Kati waingilia kati ugomvi wa koo, mapigano yasitishwa

Mapigano yamesitishwa baina ya koo Shabelle ya Kati Somalia huku viongozi wa ndani wakisema wanashughulikia kuwepo kwa mazungumzo ya amani ili kumaliza mapigano hayo yaliyosababisha vifo.
  • Wanawake na watoto waliokimbia makazi yao kutokana na vita vya koo wamepewa makazi ya muda katika uwanja wa ndege wa Jowhar, kama inavyoonekana hapa hapo tarehe 16 Novemba. [Na Osman Mohamud/Sabahi] Wanawake na watoto waliokimbia makazi yao kutokana na vita vya koo wamepewa makazi ya muda katika uwanja wa ndege wa Jowhar, kama inavyoonekana hapa hapo tarehe 16 Novemba. [Na Osman Mohamud/Sabahi]
Mapigano yalizuka mapema mwezi huu baina ya koo za Abgal na Sindle, yaliyosababisha zaidi ya vifo vya watu 20, 30 kujeruhiwa na mamia kukimbia makaazi yao, alisema Gavana wa Shabelle ya kati Yusuf Abdi Abdulle.
Mapigano hayo kwanza yalizuka katika eneo la Gedo Barkan karibu na Jowhar kutokana na mzozo wa ardhi ya kilimo. Wakaazi waliiambia Sabahi kwamba mzozo ulizidi wakati watu wenye silaha walipochoma moto ulioharibu ardhi ya kilimo na nyumba katika vijiji saba vya eneo hilo.
Hata hivyo, pande hizo mbili zilikubaliana kusitisha mapigano hapo tarehe 17 Novemba kulikopangwa na utawala wa Shabelle ya Kati, Abdulle aliiambia Sabahi.
Ili kuimarisha usitishaji mapigano hayo, utawala wa mkoa uliwaalika wabunge kutoka eneo hilo kushiriki katika mkutano wa maridhiano huko Jowhar, mji mkuu wa Shabelle ya Kati. Mkutano huo ulipangwa kuanza tarehe 19 Novemba na kudumu kwa siku tatu, lakini ulisitishwa kwa muda usiojulikana, Abdulle alisema.
Mkutano ulicheleweshwa kwa sababu bado tuko kwenye mazungumzo na koo na tunajaribu kuwashawishi kukutana ana kwa ana kwa vile lengo la kufanya mkutano huo lilikuwa kufikia maridhiano," alisema.
Serikali ya shirikisho pia imekuwa ikijihusisha katika juhudi za kuleta amani, lakini Wizara ya Mambo ya Ndani bado haijajibu maombi kutoka utawala wa mkoa wa kupeleka ujumbe kwenye mazungumzo ya amani huko Jowhar, kwa mujibu wa Abdulle.
"Tutaungwa mkono katika juhudi za kuleta amani baina ya koo zinazopigana na wazee wa kimila kutoka koo hizo na tunataka koo zote zinazopigana kuhudhuria mpango wa kuleta amani ambao tumewafikishia," Abdulle alisema. "Tuna matumaini makubwa kwamba suluhisho la amani litafikiwa na wao."

'Sijui kama wako hai au wamekufa'

Familia ambazo zimesambaratika kutokana na mapigano hayo zilipewa makazi ya muda katika Uwanja wa Ndege wa Jowhar, ambako Misheni ya Umoja wa Afrika nchini Somalia (AMISOM) imewapa hifadhi ndani ya mahema ya watu waliohamishwa, Abdulle alisema.
"Tunayashukuru majeshi ya AMISOM kwa msaada waliotoa kwa umma, ambao umekimbia mzozo wa kutumia silaha baina ya koo huko Jowhar," alisema. "Kipaumbele chetu cha kwanza ni kutafuta njia ya watu hao kurejea katika makwao kwa njia ya amani."
Mmoja wa watu waliokimbia makazi, Sahra Guled mwenye umri wa miaka 39, alitoroka na watoto wake sita kutoka Jiliyale, kijiji ambako mapigano baina ya koo za Abgal na Sindle yalianza.
"Nina furaha kwa habari nzuri niliyosikia kwamba kuna mazungumzo yanayoendelea ya maridhiano baina yao," Gulled aliiambia Sabahi. "Watoto hawazaliwi wakati wa vita, wanakufa wakati wa vita. Na mimi ninatoa wito kwa ndugu zangu, koo, kuzingatia umuhimu wa amani na kukumbatia amani na kuishi kwa pamoja."
Ili kutoroka mapigano, alikimbia yeye na familia yake kuelekea Jowhar, lakini walipata shida kufika huko kwa sababu ya mafuriko kutoka Mto Shabelle.
"Mapigano hayo yalianza wakati tulipokuwa tumevunjika moyo kuhusu mafuriko ya Mto Shabelle na tuliogopa maji yangetufikia," alisema. "Kila mtu mara moja akajiingiza katika mpango wa kuokoa maisha yake. Mungu asifiwe, sasa tuko salama na tungependa kurejea katika makazi yetu ikiwa makubaliano ya kweli yatafikiwa."
Lakini Asha Ahmed, mwenye umri wa miaka 45 na mama wa watoto tisa, yeye hakubahatika.
Alikimbilia Jowhar kutoka kijiji cha Gedo Barkan akiwa takriban na familia yake yote, lakini wapi waliko watoto wake wawili bado hakujulikani.
"Mapigano hayo yalianza wakati watoto wangu wawili walikuwa nje kuenda kuwaleta nyumbani baadhi ya mbuzi ambao walikuwa malishoni, na mpaka sasa sijui iwapo wako hai au wamekufa, kwa sababu nilimudu kwa taabu kuokoa watoto wangu wengine tu," Ahmed aliiambia Sabahi. "Nina huzuni kweli kweli kuhusu hali yao na hakuna mtu aliyeweza kunisaidia kuwatafuta ka sababu kila niliyemjua alikuwa alitoroka mapigano hayo."

Related Posts