Mataifa yenye nguvu duniani leo yamefikia makubaliano na Iran kuhusu mpango wake wa nyuklia. Kiongozi wa mazungumzo hayo Catherine Ashton pamoja na Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Iran Mohammed Javad Zarif wamethibitisha hayo mapema leo kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter.
Tangazo hilo limetokea baada ya zaidi ya siku nne za mazungumzo jijini Geneva baina ya Iran na Marekani, China, Urusi, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani yaliyosimamiwa na mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Catherine Ashton. Mazungumzo hayo yalilenga kuishawishi Iran kusitisha mipango yake ya nyuklia na badala yake kuondolewa vikwazo vya kiuchumi ilivyowekewa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na nchi za magharibi. Mkutano huo ulikuwa wa tatu jijini Geneva tangu Hassan Rouhani alipochaguliwa kuwa rais wa Iran mwezi Agosti.
Mawaziri wa Kigeni wa kigeni kutoka mataifa sita yenye nguvu waliwasili mjini humo jana Jumamosi baada ya wajumbe wa mkutano huo kupiga hatua muhimu. Rais wa Marekani Barack Obama anatarajiwa kutoa taarifa kuhusiana na makubaliano hayo baadaye leo.
habari na dw.de

