Wanajeshi waliohukumiwa maisha jela wakata rufaa


Wanajeshi wa kenya wakiwa kazini mjini Nairobi September 23, 2013.
Wanajeshi wa kenya wakiwa kazini mjini Nairobi September 23, 2013.Wanajeshi 26 wa Kenya waliohukumiwa kifungo cha maisha jela kwa kukutwa na hatia ya kutoroka eneo la kazi miaka saba iliyopita wamenyimwa dhamana. Wanajeshi hao walikuwa wamekata rufaa ya kupinga hukumu hiyo.Mahakama ya kijeshi nchini Kenya iliwahukumu wanajeshi hao kutumikia kifungo cha maisha jela mapema mwaka huu kwa madai ya kuacha kazi katika jeshi la taifa na kwenda kufanya kazi katika mataifa ya nje ikiwemo Kuwait, Iraq, na Afghanistan.Jaji Martin Muya aliwashauri wanajeshi hao pamoja na mawakili wao kusubiri rufaa ya kupinga hukumu ya kifungo cha  maisha jela itakayosikizwa mwezi Aprili.Jeshi la Kenya lilifungua mashtaka dhidi ya wanajeshi hao wakiwa ni sehemu ya wanajeshi  wengi waliodaiwa kuacha kazi jeshini.Jeshi la KDF liliwataja wanajeshi hao kuwa ni “Watoro” na hatimaye mahakama ya kijeshi ikawahukumu kifungo cha maisha.
Lakini wanajeshi hao kupitia mawakili wao waliikosoa taarifa  ya jeshi wakisema kuwa walistaafu kisheria kabla ya kuacha kazi jeshini mwaka wa 2007 na 2008 na kupata kazi ya kandarasi nchini Iraq, Kuwait na Afghanistan.
Wanajeshi wa KDFWanajeshi wa KDF
Sababu nyingine waliyoieleza ni kwamba walishtakiwa kwa sheria ya Kenya ya mwaka 2010  ilhali makosa yanayotajwa katika kesi yalitendeka siku za nyuma kuanzia mwaka 2007. Pia walielezea mashaka juu ya uhalali wa kesi hiyo wakisema walipoondoka nchi  haikuwa vitani.
Familia za wanajeshi hao zimekuwa mara kwa mara zikifika mahakamani mjini Mombasa kutaka kufahamu hatma ya jamaa zao.
Takriban wanasheria 10 waliungana kuwatetea wanajeshi hao dhidi ya makosa ya jinai yanayowakabili ikiwa  zaidi kuwatetea dhidi ya hukumu ya maisha gerezani.
Mwaka wa 2014 mahakama hiyo iliarifiwa kuwa wanajeshi wa Kenya wapatao 800 walitoroka jeshini hasa wale waliopelekwa nchini Somalia.