UNHCR Yataka Ulaya Kupokea Wahamiaji



Kasmishna mkuu wa Idara ya Umoja wa Mataifa (UNHCR) inayowashughulikia wakimbizi Antonio Guterres ameuomba umoja wa ulaya kuwapokea wakimbizi 200,000.
Amesema kupokelewa huko kuwe chini ya mradi mkubwa wa kuwapatia makazi  ili kupunguza wimbi la  wahamiaji wanaofika kwenye mipaka ya nchi za Umoja wa Ulaya ili kutafuta hifadhi.
Mkuu huyo wa UNHCR  ametoa taarifa mapema Ijumaa akiomba Umoja wa Ulaya kutekeleza mradi ambao utahitaji ushirikiano wa  mataifa yote ya Umoja wa Ulaya.
Guterres amesema mataifa ya Ulaya yatapaswa kusaidia wakimbizi kwa kuwapatia hifadhi zinazostahiki.
Wakati huo huo Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, amebadili msimamo wake Ijumaa na amesema kuwa nchi yake itawakaribisha maelfu ya wakimbizi zaidi.
Bwana Cameron, amesema wakimbizi ni wale kutoka Syria, na zaidi ya wale 5000 waliokwisha pokelewa hadi sasa.
Pia amesema hio ni kutokana na kuongezeka kwa janga na mateso wanopitia wakimbizi.
Kauli hiyo ilikuwa ni  baada ya kufanya mkutano na Waziri Mkuu wa Ureno huko Lisbon, Ureno.