MJIENDELEZE MSIISHIE HAPO MLIPOFIKIA-MWAKYEMBE


Waziri wa Mambo ya Katiba na Sheria Dkt Harrison Mwakyembe (pichani akiongea) amewataka wahitimu wa astashada na stashada za Sheria wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kujiendeleza zaidi kielimu ili waweze kwenda na wakati hasa ikizingatiwa kuwa dunia ya sasa inataka kujiendeleza kila siku vinginevyo wataachwa nyuma.
Mhe. DKT Mwakyembe ametoa rai hiyo alipowatunuku vyeti vya Astashahada na Stashahada wahitimu hao katika ukumbi wa Jaji Nyalali uliopo chuoni hapo mjini Lushoto.
Amewataka wahitimu hao kuwa tayari kulihudumia taifa kwa kufanya kazi kwa moyo na kuepuka kujihusisha na vitendo vya rushwa kwa kuwa rushwa ni adui mkubwa wa haki duniani
Amewataka wahitimu hao kuwa tayari kuwahudumia wananchi katika eneo hilo hasa ikizingatiwa kuwa serikali iko mbioni kutunga sheria ya ahuduma ya msaada wa kisheria ambayo itawawezesha wananchi wenye uhitaji kupata huduma za kisheria kupitia wasaidizi wa kisheria.
"Niwaambie ninyi mliohitimu hapa leo mna bahati sana, Serikali sasa inatunga Sheria ya Msaada wa huduma za kisheria , umeshasomwa Bungeni kwa mara ya kwanza na Bunge likiupitisha na kuwa Sheria mtaweza kufanya kazi kama wasaidizi wa sheria na hivyo kuwahudumia wananchi wengi wenye uhitaji na kusaidia harakati za utoaji haki nchini," alisema Dkt Mwakyembe
Amesema kutungwa kwa sheria hiyo kutawawezesha wahitimu hao kuwa na uwezo wa kuwahudumia wananchi kwa kuwapa msaada wa kisheria wananchi hasa wale wasio na uwezo wa kumudu gharama za mawakili.
Dkt Mwakyembe ametunuku vyeti vya astashahada kwa wahitimu 135 na stashahada kwa wahitimu 208 katika Mahafali ya 16 ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama kilichopo Lushoto mkoani Tanga
Wakati huo huo Chuo hicho cha IJA kimezindua NEMBO yake , Tovuti mpya ya Chuo na mfumo wa mawasiliano kwa barua pepe kutumia mtandao wa Serikali. 
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa vitu hivyo Mkuu wa Chuo hicho Mhe. Jaji Dkt Paul Kihwelo alisema  sio kwamba Chuo hakikuwa na Nembo na Tovuti ila yanefanyika marekebisho makubwa katika vitu hivyo ili kwenda na wakati.

Alisema kwamba  Chuo ndio kimeanza  kutumia barua pepe kwa kutumia mtandao wa Serikali ambapo kwa sasa utawahusu watumishi wa chuo hicho kama ilivyo kwa taasisi nyingine za Serikali na wanatarajia pia kuwaunganisha wanafunzi hapo baadae