Mbeya Press yafungwa kwa taabu

Na Mwandishi wetu,Rungwe.

TIMU ya soka ya waandishi wa habari mkoa wa Mbeya(MBPC FC) mwishoni mwa wiki ilijikuta inanyukwa kwa taabu goli 3-0 na timu ya kata ya Kisondelo iliyopo wilayani Rungwe katika mchezo wa kirafiki uliopigwa kijijini Lutete wilayani hapo.

Katika mchezo huo MBPC FC iliweza kutawala mchezo katika dakika 45 zote za kwanza japo haikuweza kutamba katika lango la wapinzani wao kwa kufunga hata goli moja lakini hadi mapumziko hakuna timu iliyokuwa imethubutu kutikisa nyavu za mpinzani wake.

Kipindi cha pili kilianza kwa MBPC kuonesha uhai katika dakika kumi za kwanza lakini baada ya hapo mabadiliko ya wachezaji kadhaa yaliyofanywa na timu ya kaya yaliionesha kudhoofisha kwa kiasi kikubwa uapnde wa kiungo wa timu ya wanahabari na  hapo ndipo hali ya mchezo ilibadilika na wanahabari kuwa katika wakati mgumu.

Timu ya kata ya Kisondela ilianza kujipatia goli la kwanza kunako dakika ya 60,goli la pili likapatikana dakika ya 72 na la tatu dakika ya 80 ya mchezo.

Akizungumzia kufungwa kwa timu ya MBPC FC mwenyekiti wa kamati ya michezo na burudani,Joachim Nyambo alisema zipo sababu nyingi zilizopelekea timu yake kupata matokeo hayo ikiwemo uchovu na pia baadhi ya wachezaji tegemeo kutokuwepo kwenye msafara huo.

“Sote tunatambua wachezaji wameingia uwanjani wakiwa na uchovu wa safari ya kutoka jijini Mbeya mpaka hapa kijijini Lutete.Tulihitaji kupata muda kwaajili ya mapumziko lakini tumefika leo na kucheza mechi.Ilikuwa vigumu kutoka na ushindi”

“Lakini pia kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ya msiba wa mwanahabari mwenzetu Jane Lawa baadhi ya wanahabari wameshindwa kujumuika nasi katika msafara huu kwakuwa wamelazimika kubaki kwaajili ya kuupokea mwili wa marehemu unaosafirishwa kutoka jijini Dar es salaam hadi jijini Mbeya.Kati ya wanahabari waliobaki jijini wamo pia wachezaji ambao kimsingi ni tegemeo kwenye timu yetu.Ndiyo sababu utaona hapa uwanjani tumekosa hata mchezaji mmoja wa akiba” alisisitiza Nyambo.

Kwa upande wao wakazi wa kata ya Kisondelo waliipongeza timu ya MBPC FC wakisema walitarajia ingekuwa timu rahisi kuifungwa kwakuwa wachezaji wake ni watu wenye majukumu mengi lakini walionesha upinzani wa kutosha kwenye mchezo huo.

Mmoja wa wakazi hao Jonas Mwasumbi ambaye pia ni mwanahabari mkongwe alisema ujio wa timu ya wanahabari imeleta chachu kimichezo kwenye kata hiyo kwakuwa jamii ya eneo hilo sasa inatambua kuwa wanahabari hawaishii kuandika na kutangaza habari za michezo bali pia wanao uwezo wa kushiriki kwa vitendo.