HIITI, BRIGHTON WATWAA TUZO KILIMANJARO MARATHON MWAKA HUU

WANARIAZA Nicodemus Hiiti na Banuelia Brighton wametwaa taji la ushindi katika Mbio za “Mt. Kilimanjaro Marathon” zilizofanyika jana mjini Moshi wakiwatupa wamarekani walioshiriki mbio hizo.

Nicodemus (Arusha) na Banuelia Brighton (Moshi) walikimbia kilometa 42 kwa muda wa saa 2:39.40 na 3:12.22.
 
Klabu ya Holili Youth Athletics (HYAC) katika mbio hizo za kilometa 42 iliweza kuchukua nafasi za pili na tatu zilizokwenda kwa Andrew Boniface (2:39.09) na Procesius Prosper (2:39.10).

Nafasi ya pili kwa wanawake ilichukuliwa na Nicole Greene kutoka Marekani aliyekimbia kwa muda wa saa 3:52.16. mmarekani mwingine kwa wanaume alikuwa Chad Greene aliyemaliza nafasi ya 4 kwa muda wa 3:43.52.

Kilometa 21, wanaume katika Mt. Kilimanjaro Marathon ilichukuliwa na Pascal Mombo (HYAC) aliyekimbia kwa muda wa saa 1:08.16, akichuana vikali na Elibariki Buko (1:08.24) na Oswald Kahuruzi (1:08.40) wote kutoka klabu hapo.

Kwa upande wa wanawake  Kilometa 21 ilichukuliwa  na wanariadha kutoka HYAC ambao ni Furaha Sambeke aliyekimbia kwa muda wa saa 1:25.40, Irene Chima (1:32.15) na Neema Mathias (1:36.20); huku mmarekani Nancy Loughlin akiingia wanne (1:46.04).

Pia kulikuwepo na mbio za kilometa 10 ambapo Hilary Hendry alishika nafasi ya kwanza akifuatiwa na Ottoman Seki kwa wanaume waliokimbia kwa dakika 68.10 na 74.20.

Adelina Audax na Lidiuna Godfrey kutoka HYAC walimaliza mbio hizo wakikimbia kwa muda wa dakika 52.30 na 52.33 huku nafasi ya tatu ikienda kwa Glory Mbise aliyekimbia kwa muda wa dakika 53.24; wamarekani Hilary Hendron (Tenessee) na Susan HawkesTeeter (New York) walimaliza kwa dakika 61.42 na 68.15

Mratibu na Mwasisi wa Mbio hizo Mama Maria Frances (Washington DC) aliwataka watanzania kuendelea kuutangaza Mlima Kilimanjaro kutokana na ukweli kwamba umekuwa ukitumika kuwanufaisha mataifa mengine.

Aliongeza kuwa wanariadha wanapaswa kujituma wanapokuwa katika mazoezi ili kuleta ufanisi wakati pindi michuano inapokuja hivyo kutoa mwangaza wa maisha ya mwanariadha kimataifa.

Mbio hizo zilifanyika mjini Moshi zikitimiza miaka 23 tangu kuasisiwa kwake mwaka 1991 zikiwa na malengo ya kuutangaza mlima Kilimanjaro kuwa ni kivutio cha kipekee.

Related Posts