Miaka mitatu hawajasomewa mapato na matumizi

WAKAZI wa Kijiji cha Mkwajuni Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya
wamelalamikia utendaji mbovu wa viongozi wao ikiwemo kushindwa kusoma
taarifa ya mapato na matumizi kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo
iliyopita.


Baadhi ya wakazi wa vitongoji vya Mkwajuni ''A'',  Mkwajuni ''B'',
Mnazi Mmoja,  Kamficheni ''A'' na Kamficheni ''B'' katika Kijiji Mama
cha Mkwajuni, wamesema  wanafikiria kususia michango ya shughuli za
maendeleo ya kijamii kijijini hapo kwa sababu taarifa za michango hiyo
hazipo wazi.


Wameituhumu ofisi ya kijiji hicho kushindwa kutoa taarifa za mapato na
matumizi katika kipindi cha miaka mitatu mfululizo iliypita kitendo
ambacho kimeibua hisia mbalimbali kwa wakazi hao na kufikia uamuzi wa
kutaka kugoma kuendelea kuchangia michango mbalimbali kama uongozi
utaendelea kukaa kimya bila kusoma taarifa hiyo ya Serikali ya Kijiji.


Mwenyekiti wa Kijiji hicho Credo Kayanza akizungumza kwa njia ya simu
amekanusha taarifa hizo kwa maelezo kwamba katika uongozi wake kijiji
chake kinashika nafasi ya kwanza katika Kata ya Mkwajuni kusoma
taarifa za mapato na matumizi ya serikali ya kijiji.


Kayanza alisema kwa mara ya mwisho alisoma taarifa hiyo mnamo mwezi wa
Agosti mwaka jana jambo ambalo wananchi wake wamelikanusha na
kufafanua kuwa kwa mujibu wa kanuni za utawala Bora na wa Kidemokrasia
taarifa hizo zinapaswa kusomwa kwenye mikutano ya hadhara jambo ambalo
halijafanyika katika kipindi hicho.

Mbali ya tuhuma hiyo, wakazi wa maeneo hayo wamezitaja dosari zingine
za kiutendaji kijijini hapo kuwa ni pamoja na kukaidi agizo la Mkuu wa
Wilaya ya Chunya, Deodatus Kinawiro ambaye mwaka jana  aliuagiza
uongozi kuomba vibali vya kuvuna mbao kwa ajili ya kutengenezea
madawati ili kuondokana na kero ya upungufu wa madawati kwa wanafunzi
wa kata hiyo, hakuna utekelezwaji wa agizo hilo.

Mwenyekiti amekiri kukaidi agizo hilo kwa sababu alizozitaja kuwa
hajafuatilia kibali kutokana na kijiji hicho kukosa misitu ya kuvuna
mbao, hata hivyo sababu hizo zinaonekana ni kinyume na kusudi la Mkuu
wa Wilaya ambaye aliruhusu wapatiwe kibali cha kuvuna mbao mahali
popote ndani ya wilaya hiyo.


Diwani wa kata ya Mkwajuni Chesco Ngailo hajapatikana mara moja
kuzungumzia suala hili hata hivyo wananchi wana haki ya kusomewa
taarifa za mapato na matumizi kila mwaka.