Waathirika wa ubakaji watoa kauli


Na Haji Nassor, Pemba
Waliobakwa na kisha kuozwa waume katika wilaya ya Wete mkoa wa kaskazini Pemba, wamesema ndoa za mkeka zinazofungwa kama sulhu, zinachangia kwa kiasi kikubwa kasi ubakaji katika jamii.

Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi, umeonesha jamii imekuwa na uharaka wa kuwafungisha ndoa mara wanapobaini kuwepo vitendo hivyo,wakidhani ndio sulhu ya kuvitokomeza badala yake vimekuwa vikichangia kuongezeka.

Uchunguzi umebaini imekuwa na kawaida kuharakia sulhu ya ndoa, hata kama shauri hilo limeshafikishwa katika vyombo vya sheria, jambo ambalo huwapa jeuri na kiburi wabakaji.

Mmoja kati ya waathirika wa ubakaji na kisha kuolewa mwenye miaka 17, mkaazi wa shehia ya Mchangamdogo wilayani humo, alisema binafsi baada ya kujihisi ameshapewa ujauzito, alikimbilia kituo cha polisi na kisha muhusika kukamatwa.

Awali, alimueleza mpenzi wake huyo kwamba, ameshampa ujauzito na alipokataa, ndipo alichukua uamuzi wa kukimbilia kituo cha polisi Wete,inagwa kesi hiyo haikufikishwa mahakamani.


Nae muathirika mwengine wa vitendo hivyo, mkaazi wa shehia ya Mchangamdogo (18) ambae alikatisha masomo alisema, mara baada ya kubainika na wazazi wake kwamba ameshapata ujauzito, harakati za kuolewa zilianza.

Aliwekewa mkazo na wazazi wake na hata baadhi ya marafiki, kwamba ni vyema akakubali kuolewa na baada ya kujkifungua aliachwa.

Wazazi wa vijana hao wa kike walikiri kufanya hivyo, kutokana na kuogopa usumbufu katika vyombo vya sheria.

Kwa upande wake Mratibu wa wanawake na watoto wa shehia ya Mchangamdogo, Mbeu Makame Bakari, alisema chanzo cha vitendo hivyo ni kwa wakosaji kukosa kutiwa adabu inayofaa.

Sheha wa shehia ya Kinyikani wilaya ya Wete, Mussa Rashid Said, alieleza kuwa, chanzo cha vitendo hivyo ni kuondoka kwa malezi ya pamoja ambayo yalikuwa katika miaka ya iliopita.


Nae Mratibu wa wanawake na watoto wa shehia ya Mjini Ole, Khadija Henop Maziku, alisema, bado jamii haijaona ubakaji kuwa tatizo kutokana na kupuza pale linapotokezea katika shehia zao.