IS wapata mafanikio dhidi ya majeshi ya Syria upande wa mashariki
Kundi la Dola la Kiislamu limekamata maeneo mapya kutoka kwa majeshi ya Syria mashariki mwa mji wa Deir al-Zor leo, ikiwa ni mafanikio yake ya kwanza katika eneo hilo katika muda wa miezi miwili. Wapiganaji kutoka kila upande wameuwawa katika mapambano hayo mjini Deir al-Zor, mji ulioko kilometa 450 kaskazini mashariki mwa Damascus katika jimbo linalopakana na Iraq. Dola la Kiislamu , ambalo linalengwa katika mashambulio ya anga ya Marekani nchini Iraq na Syria , limekamata maeneo makubwa ya eneo la viwanda la Deir al-Zor, ikiwa na maana kuwa kundi hilo sasa linadhibiti zaidi ya nusu ya mji huo. Mkuu wa shirika linaloangalia haki za binadamu nchini Syria Rami Abdul Rahman amesema kundi hilo la wanamgambo wa Kiislamu , ambalo linapambana na majeshi ya Wakurdi kuudhibiti mji wa Kobani katika mpaka na Uturuki limepeka wapiganaji zaidi mjini Deir al-Zor katika siku za karibuni.
Wakati huo huo Uingereza imesema leo imeidhinisha kupelekwa ndege zenye silaha na zisizo na silaha zinazoruka bila rubani kwa ajili ya uchunguzi wa kijasusi katika anga ya Syria, ili kupata taarifa za kijasusi za kundi la Dola la Kiislamu.