Mabomu mawili yaliyotegwa katika gari katika eneo la Washia
kaskazini mashariki mwa Baghdad leo, yamesababisha vifo vya
kiasi ya watu 21. Miripuko hiyo katika eneo la kuegesha magari
katika eneo la Talbiyah, ambayo pia imewajeruhi kiasi watu 40,
ilikuwa ya hivi karibuni kabisa katika wimbi la mashambulizi ya
mabomu yanayolenga jamii ya Washia walio wengi katika mji
mkuu ambayo imesababisha watu 40 kuuwawa katika muda wa
siku tatu. Hakuna kundi lililodai mara moja kuhusika na
mashambulio hayo ya mabomu, lakini kundi la jihadi la Dola la
Kiislamu, ambalo limekamata maeneo makubwa ya Iraq tangu
mwezi Juni , limesema limefanya mashambulio mengine kama
hayo katika siku za hivi karibuni. Majeshi ya Usalama na
wanamgambo wa Kishia wamewazuwia wapiganaji wa Dola la
Kiislamu kuingia katika mji huo mkuu baada ya miezi kadhaa
ya mapigano makali, lakini wanamgambo hao bado wanauwezo
wa kufanya mashambulio ya mabomu kila siku mjini Baghdad.