Kuporomoka kwa hadhi ya mwanariadha nyota anayekimbia kwa miguu ya bandia Oscar Pistorius kutoka mwanariadha nyota wa kimataifa kumekamilika leo wakati alipopelekwa katika jela mjini Pretoria kuanza kutumikia hukumu ya miaka mitano jela.
Pistorius atakuwa mmoja kati ya wafungwa 7,000 katika gereza la Kgosi Mampuru , ambako alipelekwa saa chache baada ya kuhukumiwa kwa kumuua mpenzi wake Reeva Steenkamp katika siku ya wapendao mwaka jana. Likijulikana hapo zamani kama gereza la kati mjini Pretoria , jela hiyo inafahamika kwa ukatili dhidi ya wafungwa wa kisiasa walioshikiliwa chini ya utawala wa kibaguzi ambao ulianguka miaka 20 iliyopita.
Wakati huo huo Waafrika kusini wameeleza kukatishwa kwao tamaa na hukumu ya miaka 5 aliyopewa Pistorius , wengi wakisema amepata hukumu nyepesi kwa kumuua mpenzi wake Reeva Steenkamp. Wizara ya sheria imesema kimsingi mwanariadha huyo atatumikia miezi 10 tu jela.