Na Mwandishi Maalum, New York
Kufuatia ongezeko la makundi ya dini yenye itikadi , matukio ya kigaidi, kukosekana kuvumiliana na maridhiano, Katibu Mkuu wa wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, amewageukia viongozi wa madhebu ya mbalimbali dini duniani akiomba busara zao na uongozi wao.
Amesema, busara na uongozi wa madhehebu hayo ya dini unahitajika sana katika kuhubiri na kueneza kuvumiliana, maridhiano, stahimili, kuheshimiana na kujenga utamaduni wa kuzungumza miongoni wa jamii bila ya kujali dini zao au rangi zao.
Ban Ki Moon ametoa wito huo siku ya Jumatano hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, wakati wa mkutano wa ngazi ya juu uliojadili kwa kina kuhusu dhana ya kukuza uvumilivu na maridhiano mkazo ukiwa katika kujenga jamii yenye Amani, jumuishi na namna ya kukabiliana na vurugu zitokanazo na itikadi kali za kidini.
Mkutano huo ambao ulianza siku ya jumanne uliandaliwa na Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Bw. Sam Kutesa kwa kushirikiana na Taasisi ya Muungano wa Ustaarabu ambapo washiriki mbalimbali wakiwamo viongozi wa madhehebu ya dini walipata fursa ya kutoa tathmini ya hali ya sasa na hatari inayoikabili dunia na watu wake hasa kutokana na kukithiri kwa wimbi la machafuko na mauaji kwa visingizio mbalimbmali.
Mwakilishi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi ni miongoni mwa washiriki waliochangia majadiliano hayo ambapo alielezea uzoefu wa Tanzania juu ya namna ambavyo madhehebu ya dini ya kiislamu na kikristo yalivyoanzisha na kuenzi misingi ya majadiliano katika kutafuta suluhu na maridhiano ya changamoto mbalimbali.
Akizungumza siku hiyo ya jumatano ambapo viongozi wa madhehebu ya dini walipata fursa ya kutoa maoni, mitizamo na mapandekezo yao. Ban Ki Moon alisema:
“ Waheshimiwa viongozi wa dini, leo naomba busara zenu na uongozi wenu, kuna maeneo mawili ambayo mnaweza kuleta matokeo. Moja tunahitaji kueneza na kukuza majadiliano miongoni mwa madhehebu ya dini ili kupunguza sitofahamu na mihemuko baina ya waumini wa dini .” akasema Ban Ki Moon
Jambo la pili ambalo amelieza kuwa viongozi wa dini wanaweza kutekeleza ni kuzungumzia mazingira yanayotoa fursa kwa vikundi vyenye itikadi kali ya kushawishi na kuvutia wafuasi wapya.
Amesema Ban ki Moon , viongozi wa madhehebu ya dini, wanaupeo mkubwa wa kutambua viashiria vya uwepo wa vurugu na vuguvugu la waumini wao kurubuniwa na kuwa na mwelekeo wa itikadi kali za kidini.
“Ninawaomba mtumie ushawishi wenu wa kiroho na uadilifu , kupinga maelezo yao kwa kusimamia katika kiasi na maelewano ya pamoja. Na kuongeza. Sauti zenu ni muhimu sana katika kukemea kauli za kibaguzi na kutafuta msimamo wa pamoja”. amesisitiza katibu Mkuu
Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa, ameeleza kwamba ni vema kila mmoja wetu akajiuliza ni nini kinachoshawishi au vutia itikadi kali na ukereketwa wa kupindukia.
Akasema wengi wanaojiunga na makundi yenye itikadi kali ni vijana lakini hivi sasa kuna wimbi la wanawake wanaojiunga jambo alilosema linatisha Zaidi.
Ban Ki Moon amesema, makombora yanaweza kuwauwa magaidi. Lakini anashawishika kuamini kwamba utawala bora ndio utakaomaliza ugaidi kwa kusimamia misingi ya utawala wa sheria, haki za binadamu, kumaliza umaskini, na kuondoa pengo la kati ya walio nacho na wasionacho.
Katibu Mkuu amewaeleza viongozi hao wa dini kwamba anakusudia kuunda Jopo la washauri la viongozi wa dini na wengine litakalotoa mwongozo wa namna ya kushughulikia changamoto mbalimbali.
Aidha amebainisha kwamba baadaye mwaka huu atawalisha Mkakati wa Umoja wa Mataifa wa kuzuia vurugu zinazosababishwa na ukereketwa wa kupindukia.
Viongozi wa madhehebu ya dini waliozungumza katika mkutano huo, walisisitiza sana kuhusu umuhimu wa utoaji wa elimu na mafunzo yanayozingatia au kujielekeza katika kukuza misingi ya kustahimiliana na kuheshimiana kwa misingi ya tofauti za kidini, kiimani, uhuru wa mtu kuabudu bila ya kujali tofauti ya rangi yake au nchi anayotoka.
Wamesisitiza kwamba elimu hiyo inapashwa kutolewa kuanzia katika shule za awali hadi vyuo vikuu, jambo ambalo wanaamini kwamba kama likifanyika kwa umakini siyo tu litawaepusha vijana kujiingiza katika misimamo ya itikadi kali na ukereketwa wa kupindukia lakini pia utaifanya dunia kuwa mahali salama.
Vile vile wamesisitiza kuwa, hakuna dini yoyote inayohubiri chuki, kubaguana au kuuana, bali dini zote na vitabu vya dini vinasisitiza katika kuishi kwa upendo, Amani, kuvumiliana na kuridhiana kwa kuwa wote ni watoto wa mungu.
Vyombo vya habari ikiwamo mitandao ya kijamii pia viliguswa katika majadiliano hayo, ambapo wazungumzaji wengi walivitaka viwe sehemu ya utoaji wa elimu na kujenga misingi ya ustaarabu wa kuvumiliana na kujiepusha kuwa vipaza sauti au wasemaji au wachochezi wa itikadi kali za kidini na ukereketwa wa kupindukia