RAIS WA KURUHUSU RASIMU YA KATIBA MPYA KUCHAPWA KATIKA MAGAZETI YA SERIKALI

Kifungu 20 (2) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura 83, Toleo la 2013 inamtaka Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuchapisha kwenye
Gazeti la Serikali Rasimu ya Katiba ndani ya siku thelathini (30) baada ya kukabidhiwa rasimu hiyo na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Taarifa iliyotolewa leo na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue  inaeleza kwamba, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa 
Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, alikabidhiwa Rasimu ya Katiba tarehe 30 Desemba,  2013, na ataichapisha kwenye Gazeti la Serikali litakalotolewa Ijumaa, tarehe 24 Januari 2014.
Aidha, kifungu 22 (1) (c) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura 83,  Toleo la 2013, kinampa madaraka Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushauriana na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,  kuteua wajumbe 201 wa Bunge Maalumu la Katiba kutoka miongoni mwa majina  yanayopendekezwa kwao na makundi yaliyotajwa ndani ya Sheria hiyo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, anakusudia kukamilisha uteuzi wa Wajumbe hao baada ya kushauriana na Rais wa Serikali ya Mapinduzi  Zanzibar, mwanzoni mwa wiki ijayo na majina hayo kuchapishwa kwenye Gazeti  la Serikali kama kifungu 22 (3) cha Sheria iliyotajwa inavyomtaka kufanya.

Imetolewa na:

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu
Dar es Salaam.
22 Januari, 2014