TREVOR NOAH: WATU WALIOGAWANYIKA NI WEPESI KUTAWALIWA

Nilipoanza kuongoza kipindi cha “The Daily Show” kilichokuwa cha Jon Stewart mwaka 2015, nilishangazwa nilipojua kuwa kazi yangu haikuwa kuchekesha tu bali pia kuwashambulia (kwa wanayofanya au kutofanya), kuwapinga, kuwaponda na kuwadhalilisha wapinzani wa watetezi wa uhuru wa yaliyofikiwa na maendeleo ya Marekani. Baadhi ya watu — wengi wao wakiwa ni wanufaika wa mfumo huria wa nchi hii — walianza kunishambulia kwa kuzidisha kiwango cha kuwashambulia watu tofauti na alivyokuwa anafanya mtangulizi wangu.
Mwanzoni mwa zama za blogu, YouTube na mitandao ya kijamii, watu walikuwa wakichukua vipande vizuri zaidi vya kipindi cha Jon na kuvisambaza sana kwa kuvipa vichwa vya habari vya kuvutia na mwisho vikaanza kupoteza maana kabisa vikiwa vinajitegemea, tofauti na kuangalia kipindi kizima ambacho mtiririko wa mawazo ulikuwa umepangiliwa.
Nchini Afrika Kusini, huwa tunatumia sanaa ya ucheshi kukosoa na kuchambua maswala mbalimbali kwenye jamii, na ingawa tulikuwa hatuachi kuwaandama wanasiasa, tulikuwa hatuuani wenyewe kwa wenyewe. Kama naweza kufananisha na kitu chochote, vipindi nilivyokuwa nafanya nyumbani vilikuwa ni kwa ajili ya kufuta kumbukumbu iliyoachwa na utawala wa ubaguzi wa rangi wa apartheid — ambapo watu weusi, weupe, na wahindi wanatumia ucheshi kukabiliana na maumivu na kumbukumbu mbaya iliyoachwa na ubaguzi huo. Nchini Afrika Kusini, sanaa ya uchekeshaji inatuleta pamoja. Huku Marekani, inatugawa.
Kwakuwa mimi si mweusi wala si mzungu, nilikuwa nalazimika kuishi katikati ya mstari unaotenganisha wazungu na weusi sababu mzazi wangu mmoja alikuwa mweusi na mwengine mzungu. Nililazimika kuwasiliana na wenzangu wa upande wowote kutokea kwenye mstari huo. Nililazimika kujifunza jinsi ya kuweza kuwaendea watu, na matatizo, kwa upole – bila hivyo, nisingekuwa hai mpaka sasa.
Huku Marekani hawataki upole. Machaguo yaliyopo ni mawili tu, watu weusi ni wahalifu, au polisi ni wabaguzi wa rangi — chagua upande wako. Vita ni ‘sisi dhidi ya wao.’ Uwe pamoja nasi au adui yetu. Mawazo haya ya kitaifa yanachangiwa sana na athari za taarifa za habari za chuki zinazooneshwa kwa saa 24 kila siku, hii inachangiwa na mawazo ya wananchi wengi na kwa mfumo wa siasa za nchi. Mfumo wa sasa wa vyama viwili unaonekana kuhamasisha tofauti zetu kwa kiwango cha juu wakati hakuna hata haja ya kuwepo kwa tofauti hizo.
Swala hili halijawahi kuwa wazi sana kama kipindi cha kampeni za urais za Donald Trump. Na sera zake za kibaguzi zilizowavutia wapiga kura waliojaa woga, Trump alifanikiwa kuwagawa wapiga kura waliokuwa wametabiriwa kwamba watampigia mpinzani wake. Woga huu uliwafanya watu wasiwaze wala kujadili kuhusu ukweli kwamba Wamarekani, bila kujali wa Republican wala Democrat, walitaka mambo yale yale: kazi nzuri, nyumba nzuri, fursa za maendeleo na zaidi ya yote, heshima.
Unapokuwa na watu wenye misimamo mikali sana unakuwa unahamasisha kukwama kwa kila kitu na kurudisha nyuma maendeleo. Badala ya kuongea kwa tahadhari kuhusu mambo mengi yanayotuunganisha, tunapigiana mayowe kuhusu mambo machache sana yanayotutofautisha — jambo ambalo watu wanaopenda mamlaka kama Trump wanataka: Watu waliogawanyika ni rahisi sana kuwatawala. Hilo ndio lilikuwa lengo kubwa sana la utawala wa ubaguzi wa rangi nchini kwetu.
Kwa watu wa misimamo mikali sana na wale wanaoamini kwenye jambo lolote lile wanakuwa na mawazo kuwa na msimamo wa kawaida na kukubali mambo yanayosemwa na upande mwingine ni ishara ya kukata tamaa na kutokuwa na imani kabisa na misimamo yao, wakati ukweli ni kwamba kinyume chake ndio ukweli — misimamo ya kati inaipoza misimamo mikali na kuifanya iweze kutekelezeka. Nelson Mandela hakuwahi kuyumba juu ya msimamo wake wa “mtu mmoja, kura moja;” bila shaka, alikubali kuvumilia miaka 27 gerezani ili kulifanya wazo hili kuwa kweli. Lakini Taifa letu lilipokaribia kuingia kwenye vita vya ndani, Mandela alizungumza na raia wazungu kwa lugha ambayo iliondoa hofu zao zote na kuwahakikishia kuwa watakuwa na nafasi ndani ya nchi itakayojengwa upya. Alizungumza pia na askari weusi kwa lugha ambayo ilipoza hasira zao lakini hakudharau maumivu yao. Kama juhudi hizi za Mandela zingeshindikana, Afrika Kusini isingeweza kufanya mabadiliko ya amani kuja kwenye demokrasia.
Ukikulia katikati ya misimamo miwili kama ilivyokuwa kwangu, unagundua kwamba maisha yapo zaidi katikati na kwamba hayajaegemea upande wowote ule. Watu wengi wapo katikati, nafasi ya ushindi huwa ipo zaidi kwa watu wa katikati, na mara nyingi sana ukweli unakuwa hapo pia ukitusubiri sisi kuufikia.

from Blogger http://ift.tt/2uwR5O6
via IFTTT